Ufugaji wa Nyuki Tanzania

Ufugaji wa Nyuki wakubwa na wadogo ni ufugaji maarufu sana Tanzania kwasababu nyuki ni wadudu pekee ambao hutengeneza na kula asali.

Nyuki huishi na kufanya kazi kijamaa, Utendaji wao wa kazi hutegemeana na umri na mahitaji ya kundi husika.

Aina za Nyuki Ndani Ya Mzinga

 • Malkia wa Nyuki
 • Nyuki Madume
 • Nyuki Vibarua

Jinsi Nyuki Wanavyo Zaliana

Nyuki huzaliana kwa msimu maalum, unapofika msimu huo, kundi husika huzalisha madume ya kutosha na baadaye malkia wachache ambao wanapopevuka hujamiiana na madume.

Kundi la vibarua huwa na nyuki majike ambao sehemu zao za kike hazifanyi kazi. Hawa ndiyo watendaji wa takribani shughuli zote katika kundi.

Miongoni mwa shughuli zinazotendwa na vibarua ni kuzalisha chakula cha mabuu au malkia, ulinzi wa kundi kwa kutumia sumu inayotunga katika mwili wake.

Mara sumu hii inapokuwa tayari hufanya kazi ya kwenda kutafuta maji na chakula kwenye maua. Na inapofika wakati ambao kundi huhitaji masega basi vibarua huanza kujenga masega.

Mbinu za Ufugaji wa Nyuki

Kutokana na matokeo ya tafiti mbalimbali zilizofanywa kwa nyuki kuhusu namna anavyozalisha asali, mbinu mbalimbali zimependekezwa za namna ya kufuga nyuki.

Mbinu hizi zimelenga kumfanya nyuki azalishe asali zaidi kwa matumizi ya binaadamu na sio kwa manufaa yao (nyuki) wenyewe ambao lengo lao la kutengeneza asali ni kujiwekea chakula cha akiba kwa ajili ya wakati wa njaa.

Mara nyuki atengenezapo asali humpa changamoto mwanadamu kuamini kwamba anahitaji jitihada zaidi ili aweze kujaza nafasi inayoonekana tupu kwenye mzinga kabla ya msimu wa maua haujamalizika.

Jinsi Ya Kufanikiwa Kwenye ufugaji wa Nyuki

Kwanza ni vyema kufahamu mazingira ya mahali unapotaka kufugia nyuki wako na ni muhimu ni kuhakikisha kuwapo kwa;

 1. Mimea itoayo maua ya kutosha ili nyuki wako wasipoteze muda na nishati kubwa kutafuta chakula.
 2. Pawepo na majike karibu na iwapo hayapo basi wawekee kisima kidogo na kutumbukiza vijiti.
 3. Pawe na kivuli cha kutosha ili nyuki wasipoteze muda mrefu kupooza kiota chao badala ya kwenda kutafuta chakula.
 4. Pasiwe na njia kuu kwa vile nyuki hawapendi kelele na harufu mbaya kama moshi wa mashine, moto nakadhalika
 5. Pasiwe mahali penye tindikali la madawa kwani huweza kuwaua nyuki wakati wakisaka chakula na maji.
 6. Baada ya kuijua mimea itoayo maua vilevile ni muhimu kujua wakati au msimu ambao mimea hiyo hutoa maua. Kwa kawaida maua hutoka baada ya mvua za masika na vuli. Kwa kawaida msimu mkubwa huwa baada ya mvua za masika na wakati huo hujulikana kama msimu wa asali.
 7. Mara baada ya maua haya ya msimu wa asali yanapoanza kupuputika asali huanza kuiva kwenye mizinga au kiota. Nyuki huwa tayari wametengeneza asali na kuifunika kwa nta nyororo ili isiweze kunyonya maji (moisture) kwenye hewa.
 8. Wakati mvua zinapokaribia kuimalizika makundi ya nyuki huanza kuzaa watoto wengi ili wapatikane nyuki wengi wa kukusanya chakula, hivyo ni vyema kuzuia kujigawa kwa nyuki wakati huo.

Mfugaji akishaelewa mazingira ya ufugaji wa nyuki, inapasa aamue mahali pa kufugia nyuki na muda na kitu gani anatakiwa kufanya

Mambo Ya Kuzingatia Kwenye ufugaji wa Nyuki

Mfugaji nyuki lazima ajue jinsi ya kuweka mizinga ili nyuki waweze kuingia kwenye mzinga yake. Mara nyingi nyuki wanapoanza kuzaliana mfugaji wa nyuki asafishe mizinga yake na kuweka chambo ili waingie wenyewe

Jinsi Ya Kulina Asali

Mfugaji anashauriwa kuwa na kinga ya miiba ya nyuki. Nyuki huwa wanauma na sumu yao ni kali na yenye maumivu.

Kinga zinazopendekezwa ni kama vile ovaroli la mikono mirefu lenye rangi ya khaki, nyeupe au maziwa (usitumie lenye rangi nyeusi au nyekundu), tumia pia wavu wa usoni (Bee veil), mipira ya mikononi (Bee gloves), na viatu (Gum boots).

Pia ni vema kutumia bomba la moshi (Bee smoker). Bomba hili huwekwa kipande cha gunia au nguo ili ule moshi uweze kupulizwa kwenye nyuki na kuwafanya watulie.

Nyuki wanapoona moshi au moto jambo la kwanza hufikiria kukimbia au kuhama lakini kabla ya kukimbia ni lazima ale asali ashibe ndio aondoke.

Wakati akijishughulisha kula asali kwenye masega mfugaji anaweza kufanya kazi yake bila nyuki kumshambulia au kumghasi. Vifaa hivi vinapatikana kwenye ofisi za idara za misitu na nyuki.

Nyuki wa kiafrika wa kusini mwa ukanda wa Sahara huwa ni wakali kupita kiasi, hivyo baadhi ya wafugaji wa nyuki hulazimika kuchoma aina fulani ya majani (Ocinum) au aina fulani za uyoga (Puff balls) inayomea kwenye magamba ya miti iliyooza wakati wa mvua kujikinga dhidi ya mashambulizi ya nyuki wakati wa kulina asali.

Wengine huchovya gunia dawa ijulikanayo kama Ammonium nitrate na linapokauka huchomwa ndani ya bomba la moshi.

Vyote hivi huwafanya nyuki kulewa na kupumbaa hivyo kumwezesha mfugaji kushughulika bila wasiwasi na nyuki wake kwenye mzinga na bila kuwathiri nyuki.

Hata hivyo mfugaji anatakiwa kupata ushauri zaidi toka idara ya misitu na nyuki ili aweze kufuga nyuki kwa ubora na mafanikio zaidi.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo