Madhara Ya Betting Kwenye Maisha

Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi au changamoto za maisha watu wengi hutekwa na mambo mbalimbali hasa yale yanayohusu kupata pesa za haraka.

Nilipofanya utafiti mdogo nilibaini kuwa “njia za kupata pesa kwa haraka” pamoja na “njia za kupata utajiri kwa haraka” ni moja kati ya vitu vinavyotafutwa sana na watu kwenye mtandao.

Hii inadhihirisha uhitaji mkubwa wa watu kutaka kupata pesa, tena kwa muda mfupi.

Hivyo basi, hili limepelekea watu wengi kutekwa na michezo ya bahati nasibu wakifikiri kuwa inaweza kuwatoa katika matatizo au mahitaji yao ya kifedha.

1. Betting ni Biashara

Hakuna mtu atakayetoka China, India au Marekani ili aje Afrika kukugawia mamilioni ya bure kwa njia ya michezo ya kubahatisha ili utoke kwenye umasikini.

Kampuni za michezo ya kubahatisha zinazalisha faida kubwa tena kubwa sana ambayo hufichwa nyuma ya vijizawadi wanavyotoa kwa washindi wa michezo hiyo.

Kwa mfano watu 100,000 wakicheza mchezo mmoja kwa shilingi 20,000 pekee ni sawa na shilingi 2,000,000,000 hebu jiulize kweli katika bilioni 2 watashindwaje kutoa zawadi ya milioni 50 hata mara 5?

Naamini umeona wanavyopata faida kubwa kwenye biashara hii ambayo huwadanganya watu kuwa ni njia ya kuwatoa kwenye umaskini.

Kumbuka kuwa hivi leo biashara mbalimbali za hovyo hujificha kwenye kofia ya kutambulika kisheria na kulipa kodi.

Zipo nchi ambazo zimerasimisha biashara za madawa ya kulevya na silaha kwa kigezo cha kutambulika kisheria na kulipa kodi.

Hivyo kuwa macho na michezo ya kampuni hizi kwani ni biashara ya kuwahadaa watu watoe pesa zao.

2. Michezo Ya Kubahatisha Haina Mifumo inayoeleweka

Michezo hii haina mifumo wazi na inayoeleweka, wanakuambia cheza mara nyingi ushinde lakini hawasemi ni mara ngapi na ni kwanini wanashinda hata waliocheza mara chache.

Michezo hii huendeshwa kwa mfumo wa kompyuta wa kimahesabu ujulikanao kama probability; hivyo mtu yoyote anaweza kushinda au kushindwa.

Kutokana na sababu hii ni bora kuwekeza pesa zako kwenye kitu kingine chenye tija kuliko kuziweka kwenye michezo ya bahati nasibu isiyokuwa na uhakika.

Nimetafiti nikagundua ni afadhali hata spot betting kwani unachozingatia ni kutabiri matokeo kwa usahihi na unashinda.

3. Betting Huathiri Saikolojia

Michezo ya kubahatisha imetengenezwa kwa njia ambayo inawahadaa na kuwateka wale wanaocheza michezo hiyo. Hivyo huwafanya washindwe kuacha au kujitoa maraa baada ya kuanza kucheza hata kama hawashindi.

Kwa mfano michezo hii hukufanya ushinde kiasi kidogo cha fedha baada ya muda fulani ili uamini kuwa utashinda kiasi kikubwa kama utaendelea kucheza. Lakini hii ni mbinu tu ya kukuteka kwani utajikuta umeshacheza sh. 50,000  lakini umeshashinda sh. 5,000 pekee; huoni hapo unaibiwa?

4. Betting Hupoteza Upotevu wa Pesa na Muda

Kuna vitu vingi na miradi mingi ambayo unaweza kuwekeza muda na pesa zako na ukajipatia faida. Kwanini uchezee shilingi kwenye tundu la choo (michezo ya kubahatisha)?

Ni vyema ukawekeza pesa zako au hata ukanunua kitu cha maana ambacho kitakufaa kwenye maisha yako. Unaweza kuwekeza pesa zako kwenye mradi au ukanunua vitu kama vile vyombo na vifaa vya majumbani, vitabu au hata kuwasaidia wahitaji kwa muda na pesa zako.

5. Betting Sio suluhisho La Uhakika La Kifedha

Watu wengi hufikiri kuwa pesa nyingi au zinazopatikana ghafla ndio utatuzi wa matatizo yao. Hebu nikuulize swali, je ulishawahi kuona watu waliokuwa mamilionea lakini leo wanaomba hata ugali wa mchana? Walikuwa na maduka, magari, majumba lakini leo hawana kitu, je hivi vimekwenda wapi?

Pesa ni lazima zikutane na fikra na mikakati sahihi, ukipewa pesa nyingi leo kama huna fikra sahihi hazitakusaidia kitu.

Kwa kuwa pesa za michezo ya kubahatisha huja kwa ghafla bila kujiandaa wala kuzitolea jasho sana, watu wengi wanaopata pesa hizi huzitumia vibaya na kuishia kurudi kwenye umaskini wao.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo