
Jinsi Ya Kupunguza Gharama Ya Ujenzi wa Nyumba Tanzania ni muhimu kwasababu watu wengi wamejikuta katika hali ngumu ya kifedha au hata kukwama katika ujenzi kutokana na kushindwa kuweka mikakati mizuri ya kupunguza gharama za ujenzi.
1. Jitahidi Kuchagua Kiwanja Bora
Jinsi ya kuchagua kiwanja sahihi wa kiwanja kwa ajili ya ujenzi ni jambo muhimu sana. Watu wengi hujikuta wakitumbukia kwenye gharama kubwa za ujenzi kutokana na uchaguzi duni wa kiwanja.
Hebufikiri ukinunua kiwanja sehemu ambayo ni mkondo wa maji au udongo wake unatitia hili litakulazimu kutumia gharama kubwa zaidi ili kukifanya kiwanja hicho kifae kwa ujenzi, gharama ambazo zingeweza kuokolewa kama ungefanya uchaguzi sahihi wa kiwanja.
2. Jitahidi Kuchagua Ramani Nzuri na Rahisi
Pamoja na sababu kuwa suala hili linatokana na ukosefu wa elimu sahihi juu ya masuala ya ujenzi ramani mbaya huwagharimu watu wengi fedha nyingi na mwishowe haziwapi nyumba walizozihitaji.
Kwa mfano; ramani za nyumba za Ulaya (Hasa maeneo ya baridi) huwezi kuzijenga kwenye maeneo ya Afrika yenye joto.
Inaweza kuwa ni ramani nzuri sana lakini ikawa na vitu vingi vinavyoongeza gharama zisizokuwa za msingi. Vivyo hivyo ramani ya rafiki yako inaweza isiwe bora kwako.
Hivyo, hakikisha unachagua ramani nzuri na rahisi ambayo utaweza kuitekeleza vyema bila kukutengenezea mzigo mkubwa wa gharama.
3. Jitahdi Kufanya Utafiti wa Kutosha
Kukurupuka na kuanza kufanya jambo ni suala baya sana. Utafiti katika suala la ujenzi ni jambo muhimu sana litakalokuwezesha kupunguza gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa.
Unapaswa kutafiti yafuatayo:
- Bei za bidhaa na vifaa vya ujenzi
- Mafundi bora
- Vifaa bora na vya bei nzuri
- Teknolojia za kisasa kwenye ujenzi.
Ukitafiti kwa kina masuala tajwa hapo juu pamoja na mengine yanayohusiana nayo, kwa hakika utapunguza gharama za ujenzi ambazo zingepotea kutokana na kutokuwa na uelewa sahihi.
4. Jitahidi Kutumia Vifaa Mbadala
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia katika sekta ya ujenzi, kumekuwepo na vifaa pamoja na malighafi mbalimbali ambazo zinarahisisha ujenzi, zinaokoa gharama za ujenzi pamoja na kulinda mazingira.
Hivi leo zipo mbao maalumu, matofali au hata vifaa vya jamii ya vigae ambavyo vinaokoa gharama za ujenzi maradufu kuliko vifaa vya kawaida.
Hapo utaweza kupunguza gharama zisizo za lazima kwenye ujenzi.
5. Jitahidi Kusimamia Vyema Manunuzi na Ujenzi
Watu wengi wamejikuta wakipoteza fedha nyingi sana kwenye miradi yao, hasa miradi ya ujenzi kutokana na kukosa usimamizi mzuri.
Niimeona watu wakijenga nyumba kwa simu na kuishia kupata hasara kubwa. Fundi anakuambia leta mifuko 10 ya saruji kumbe ni minne tu inahitajika, fundi anakuambia ametumia kitu fulani kumbe ametumia kilicho dhaifu ili apate pesa yake ya mfukoni.
Ni muhimu kuhakikisha unasimamia manunuzi vyema pamoja na ujenzi kwa ujumla na si kumkabidhi fundi kila kitu.
6. Jitahidi Kuchagua Msimu Mzuri wa Ujenzi
Ni wazi kuwa majira kama vile ya mvua nyingi siyo rafiki kwa ujenzi; hii ni kutokana na sababu ya changamoto za usafirishaji wa malighafi za ujenzi pamoja na changamoto ya mafundi kutokuweza kufanya kazi wakati mvua ikinyesha.
Suala hili linaweza kutengeneza gharama za ziada ambazo hazikutarajiwa kama vile kuongezeka kwa gharama za usafirishaji pamoja na ununuzi wa vifaa kama vile turubai gharama ambazo zingeweza kuepukwa ikiwa msimu wa ujenzi ungechaguliwa vyema.
7. Jitahidi Kutafuta Fundi Sahihi
Hivi leo kuna mafundi wengi lakini si wote ni mafundi bora. Kwa ajili ya kwenda kwa mazoea au kutokana na kukosa uelewa, watu wengi wamejikuta wakitumia mafundi ambao huwasababishia gharama kubwa za ujenzi.
Hebu fikiri ukifanya kazi na fundi anayekosea kila kitu ni wazi kuwa kazi itakuwa ni kujenga na kubomoa ili kurekebisha makosa.
Suala hili litakusababishia kutumia pesa nyingi zaidi kwa ajili ya marekebisho ilihali pesa hizo ungeziokoa kama ungechagua fundi bora.
8. Jitahidi Kufanya Mambo Wewe Mwenyewe
Kuna baadhi ya mambo ambayo unaweza kuyafanya wewe mwenyewe au wanafamilia wako; mambo kama vile maandalizi ya awali ya kiwanja, kumwagilia maji sehemu iliyojengwa, kukusanya vipande vya mawe au tofali.
Kwa kufanya mambo kama haya au hata zaidi kulingana na uwezo wako utapunguza sana gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa.
9. Jitahidi Kutumia Tena Malighafi
Mafundi watakata mbao mpya ili tu kupata kipande kidogo wanachokihitaji kuliko kuunga vipande viwili pia kuvunja vunja matofali au kukatakata mabati mapya ili kupata kipande wanachotaka kuliko kutafuta kipande cha zamani kwa ajili ya eneo husika.
Hivyo basi, ili kupunguza gharama za ujenzi, hakikisha unasimamia matumizi ya rasilimali zilizobaki au zilizokwisha kutumika.
Vipande vya matofali, mabaki ya mawe, misumari ya zamani, au vipande vya bati vinaweza kutumika sehemu nyingine na kuokoa kiasi kikubwa cha fedha.
10. Jitahidi Kuzingatia Kanuni za Ujenzi
Masuala kama vile unyeshaji wa sehemu iliyojengwa kwa saruji, uchanganyaji wa saruji na muda wa ujenzi Ni baadhi tu ya mambo muhimu sana.
Kwa mfano nyumba isiponyeshwa vizuri ni lazima itapata nyufa na itatengeneza gharama zaidi za marekebisho
Pia nyumba ikilazamishwa kujengwa harakaharaka kuliko muda stahiki ni lazima itapata dosari mbalimbali ambazo zitagharimu fedha zaidi kuzirekebisha.