
Jinsi Ya kufanikiwa mapema kwenye maisha hapa Tanzania ni muhimu kufahamu ili uweze kufikia malengo ya mafanikio kwa haraka
1. Jitahidi Kusoma Vitabu
Kupitia vitabu unaweza kujifunza mambo mbali mbali kama vile:
- Njia za kukabiliana na matatizo mbalimbali.
- Njia za kufanya mambo mbalimbali kwa ufanisi.
- Jinsi ya kuboresha maisha yako.
- Hamasa kutoka kwa waliofanikiwa n.k.
- Maarifa mapya usiyoyajua.
Haya ni baadhi tu ya mambo ambayo unaweza kujifunza au kuyapata kutoka kwenye vitabu. Hivyo ikiwa unataka kuwa bora zaidi jizoeze kusoma vitabu mbalimbali kila mara.
Vitabu ni chanzo kikubwa cha hekima na Kadri unavyosoma vitabu ndivyo unavyozidi kupata hekima.
2. Jitahidi Kujifunza Lugha Mpya
Unaweza kufikiri kuwa kujifunza lugha mpya hakuna maana, lakini kuna manufaa makubwa.
Ikiwa unataka kuongeza wigo wako wa maarifa na fursa, basi huna budi kujifunza lugha mpya. Ikiwa unafahamu Kiswahili pekee, basi jifunze Kiingereza pia.
Kwa njia hii utaweza kuongeza wigo wako wa kupata fursa mbalimbali.
3. Jitahidi Kujifunza Course Mpya
Je kuna kozi mpya unayoweza kujifunza? Ikiwa ipo, chukua muda sasa ujifunze kozi hiyo. Kujifunza kozi mpya kutakuongezea maarifa na uelewa wako.
Kumbuka kuwa kozi hii haitakiwi kuwa ndefu; inaweza kuwa ni semina au warsha ya muda fulani.
4. Jitahidi Kushinda Hofu na Wasiwasi Wako
Ni wazi kuwa ili kuwa bora zaidi, ni lazima tushinde hofu na mashaka ambayo mara nyingi hutawala maisha yetu na kutupotezea mafanikio yetu.
Tukishinda hofu tutathubutu kufanya mambo kwa ajili ya kufikia malengo yetu.
5. Jitahidi Kuboresha Ujuzi Wako
Je kuna maarifa au ujuzi fulani ulio nao? Je kiwango na ubora wake kikoje? Ikiwa una ujuzi fulani hakikisha unaukuza na kuuendeleza uwe bora kabisa.
Ikiwa wewe ni mjasiriamali, mbunifu, fundi, msanii n.k. Hakikisha unajenga uwezo na maaraifa yako yawe bora kabisa.
Kila mara hakikisha unajifunza mambo mapya yanayohusiana na ujuzi wako.
6. Jitahidi Uamke Mapema
Kuamka mapema ni jambo ambalo linaweza kukufanya kuwa bora zaidi ikiwa utalifanya kwa uhakika.
Kuamka mapema kutakupa fursa ya kutumia muda vyema; hasa muda wa asubuhi ambao mwili na akili vinakuwa viko vizuri kiafya.
Kwa njia hii utaweza kuongeza tija na ufanisi katika yale yote unayoyafanya.
7. Jitahidi Kufanya Mazoezi
Mazoezi ni muhimu sana kwa ajili ya kujenga afya zetu. Unaweza kukimbia, kupiga push up, kuruka kamba, kunyanyua vyuma n.k.
Kwa njia ya mazoezi unaweza kuimarisha na kulinda afya ya mwili wako; jambo hili litakufanya kuwa bora zaidi na kuwa na ufanisi mkubwa katika utendaji wako wa kazi.
8. Jitahidi Kujiwekea Malengo
Watu wengi hawana wala hawafahamu umuhimu wa kuwa na malengo kwenye maisha yao. Malengo hukuwezesha kufahamu unataka kufanya nini, lini na wapi na kwa namna gani.
Tambua na jiwekee malengo maishani mwako, na kila siku hakikisha unafanya kitu ili kuelekea malengo yako:
9. Jitahidi Kuanza Kutenda
Mara nyingi tunazumngumza mambo mengi, lakini tunayoyaweka kwenye matendo ni machache. Nianze kwa kukuuliza swali, je utaweka mambo haya unayoyasoma hapa kwenye matendo?
Ili kuwa bora zaidi ni muhimu kuweka kwenye matendo yale tunayoyawaza na kuyapanga. Haitoshi tu kuwaza na kupanga, bali tunatakiwa tuyafanyie kazi.
Ikiwa ni mpango wa biashara, mradi, au aina nyingine ya uwekezaji basi inatakiwa kuanza kuuweka kwenye matendo.
10. Jitahidi Kujifunza Kwa Watu Unaowapenda
Kila mtu ana watu wake wanaomhamasisha juu ya mafanikio maishani mwake. Hivyo ili kuwa bora zaidi ni muhimu kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa watu hawa.
Unaweza kujifunza walivyoanza, walivyokabili changamoto, wanavyotekeleza mipango yao n.k. Kwa kufanya hivi utapata hamasa na mwongozo wa kutekeleza mipango yako mbalimbali.
11. Jitahidi Kuacha Tabia Mbaya
Kuna tabia nyingi, lakini siyo tabia zote ni nzuri. Bainisha tabia ambazo hazikujengi kwenye maisha yako na uziache mara moja.
Tabia kama vile starehe na anasa, uvivu, matumizi mabaya ya pesa n.k. kamwe hazitakufanya kuwa bora zaidi.
12. Jitahidi Kutumia Muda Vizuri
Kanuni moja muhimu ya kufanikiwa na kuwa bora zaidi ni matumizi mazuri ya muda. Hakikisha unajipangia ratiba nzuri na unaifuata.
Epuka vitu, tabia na watu ambao wanakusababisha upoteze au usitumie muda wako vyema. Hakikisha siku inapomalizika una ujasiri wa kuweza kuorodhesha vitu ulivyokamilisha.
13. Jitahidi Kuishi na Watu Vizuri
Hakuna haja ya kutengeneza uadui au mgawanyiko usiokuwa na sababu kati yako na watu wengine. Heshimu, thamini, samehe na jali kila mtu.
Kuishi na watu vizuri kunakufanya kuwa bora zaidi kwani kutakujengea upendo na thamani kati ya wale unaoishi nao.
Unaweza usione thamani ya jambo hili, lakini hebu jaribu kuliweka katika matendo baada ya kusoma makala hii nawe utaona matokeo.
14. Jitahidi Kuepuka Watu Walioshindwa
Mara nyingi tunazungukwa na watu walioshindwa kuliko wale waliofanikiwa. Watu hawa wamejaa maneno mengi yenye visingizio na kulaumu kila kitu.
Watu walioshindwa hutetea kushindwa kwao, hupuuza mafanikio ya wengine, hukatisha watu tamaa na hata kulalamikia kila kitu hadi hali ya hewa.
Hivyo hatuna budi kuwaepuka watu hawa ili wasije wakatukwamisha katika kufikia malengo yetu. Ili kuwa bora zaidi ni muhimu kutambua ni watu gani wakuwa karibu nao maishani mwetu.
15. Jitahidi Kupata Muda wa Kupumzika
Ingawa tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii; swala la kumpumzika ni muhimu sana. Kupumzika hufanya miili yetu kujijenga na kurudisha nguvu iliyotumika wakati wa kazi mbalimbali.
Ni muhimu kutenga muda wa kutosha wa kupumzika ili tuweze kuwa bora zaidi. Kumbuka gari haliwezi kwenda bila kuwa na mafuta nguvu na afya njema ndiyo mafuta ya miili yetu.