Tabia za Mafanikio Kwenye Maisha

Kila jambo tunaloliona kwenye ulimwengu wa leo lilianza kwanza kwenye fikra. hauwezi kufanikiwa ikiwa hautoona lile unalotaka kulifanya au kulifanikisha akilini mwako kwanza.

1. Amini Kuwa Kila Kitu Kinawezekana

Hakuna mtu yeyote anayeweza kuwa mshindi bila kuamini kwanza kuwa kila kitu kinawezekana. Ikiwa hauamini kuwa kila kitu kinawezekana, utawezaje kufanya mambo kwa bidii na kwa imani kuwa yatafanikiwa?

Hebu fikiri juu ya watu waliofanya safari ya kwanza kwenda mwezini; ni wazi kuwa hakukuwa na safari yoyote iliyofanyika na kufanikiwa kabla ya hapo, lakini waliamini safari yao ya kwanza itafanikiwa na ikawa hivyo.

2. Jitahidi Kusamehe Kila Mtu

Kusamehe kuna faida kemkem, moja wapo ni kukufanya uwe huru katika fikra zako na uweze kufikiri kama mshindi. Utawezaje kufikiri na kupanga mikakati ya maendeleo wakati moyo na fikra zako zimejaa uchungu na ghadhabu dhidi ya wale waliokuudhi?

Samehe ujipe nafasi ya kulinda afya ya mwili wako na nafsi yako samehe ujipe nafasi ya kufikiri kama mshindi na si kama aliyejeruhiwa.

3. Jitahidi Kujifunza Kitu Kipya Kila Siku

Ikiwa unataka kufikiri kama mshindi, ni lazima ujizoeze kujifunza kitu kipya kila siku. Iwapo utajifunza kitu kipya kila siku utanufaika kwa mambo kama vile:

  • Kufahamu njia za kukabili matatizo ya kila siku.
  • Kufahamu fursa mpya za kuboresha maisha yako.
  • Kupata hamasa kutokana na vitu vilivyokamilishwa na wengine.
  • Kujifunza njia za kuboresha na kulinda afya yako.

Kama kujifunza vitu vipya kuna manufaa hivi kwanini wewe upuuzie hili?

Nikushuhudie kuwa swala hili limeniwezesha kufahamu mambo mengi sana kwenye sekta ya TEHAMA (IT), kwani nimejizoeza kujifunza kitu kipya kila mara ili kupanua uelewa wangu.

4. Jitahidi Kuacha Kulaumu

Washindi siyo watu wa kulalamika na kulaumu vitu na watu. Kuna watu ambao wao kutwa kuchwa ni kulaumu na kulalamika, ooh! hii serikali, aah! hii kazi, ooh! hii familia, aah! huyu mume au mke.

Mtu analaumu na kulalamikia watu na vitu akidhani kuwa kwa njia hiyo atatatua matatizo yanayomkabili. Ni hakika kuwa siku zitapita na matatizo yake yatazidi na atabaki katika hali hiyo hiyo ya kushindwa.

Hivyo, ukitaka kuwa mshindi au kufikiri kama mshindi basi epuka kulalamika na kulaumu kuanzia sasa.

5. Jitahidi Kuepuka Kukata Tamaa

Pasipo shaka mwanamichezo mashuhuri Dan O’Brien alifahamu wazi kuwa iwapo mtu hatokata tamaa atafanikiwa katika kila jambo analolifanya. Kukata tamaa ni sumu ambayo imewakwamisha watu wengi.

Mtu anapokutana na changamoto na kukata tamaa na kuacha kufanya kile anachokifanya, ni wazi kuwa hatoweza kufikia malengo yake.

Kila mara kumbuka kuwa safari ya mafanikio ina changamoto ambazo zinahitaji uvumilivu ili kuzivuka.

6. Jitahidi Kuwaepuka Watu Walioshindwa

Tabia kubwa ya watu walioshindwa ni kuwafanya wengine washindwe kama wao au kuwafanya wafikiri kama watu walioshindwa badala ya kufikiri kama washindi.

Watu walioshindwa wana maneno mengi na matendo mengi ya kukufanya ufikiri kama wao ili ushindwe kuliko kushinda katika lile unalolifanya.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo