
Ukweli ni kuwa kufundisha na kuwaelewesha watu wengine kwenye maisha ni swala lenye manufaa mengi ambayo watu wasiofanya hivyo wanayakosa.
1. Kuwasaidia Watu Huongeza Maarifa
Kufundisha wengine ni njia bora ya kuongeza maarifa yako. Kwanza kabisa utahitajika kujiandaa kwa kusoma na kujifunza mambo mbalimbali ili uweze kufundisha vyema, hili litakuongezea kiwango kikubwa cha maarifa.
Pili wakati wa kufundisha utajifunza mambo mbalimbali kutoka kwa yule unayemfundisha au wale unaowafundisha kwani nao kuna mambo wanayoyafahamu tofauti na wewe.
2. Kuwasaidia Watu Hufundisha Mipango
Ili uweze kufundisha vyema ni lazima upangilie na kuandaa kile utakachofundisha. Kwa njia hii utajifunza kupanga na kuandalia somo au mada yako kabla ya kuiwasilisha.
3. Kuwasaidia Watu Huboresha Uwezo wa Mawasiliano
Utahitaji kuwasiliana na wale unaowafundisha ili wapate kile unacholenga kuwafundisha. Kwa njia hii utaboresha uwezo wako wa kuwasiliana.
Hili linahusisha pia kuboresha uwezo wako wa uandishi pamoja na uwezo wa kuzungumza mbele za watu ikiwa utakuwa unafundisha ana kwa ana.
4. Kuwasaidia Watu Husaidia Kujitathimini
Njia bora ya kujitathimini ni kwa kufundisha watu wengine kile unachokijua kisha uwaruhusu wakupe tathimini ya uwezo wako.
Kwa njia hii utatambua ni jambo gani unalolifanya kwa ubora na ni wapi unapofanya kwa udhaifu ili ufanye maboresho zaidi.
5. Kuwasaidia Watu Hukuwezesha Kutatua Matatizo
Kuwafundisha watu mambo mbalimbali ni njia bora na ya gharama nafuu ya kutatua matatizo yao. Hebu fikiri unamfundisha mtu jinsi ya kujikinga au kutibu maradhi fulani, akifanyia kazi maarifa hayo na kuona matokeo tayari utakuwa umetatua tatizo lake.
Kwa mfano pia unaweza kumfundisha mtu jinsi ya kujikwamua kiuchumi na akatoka kwenye matatizo ya kifedha; kwa njia hii utakuwa umefanya jambo kubwa kuliko hata kumpa pesa.
6. Kuwasaidia Watu Hutengeneza Kumbu Kumbu
Ni vigumu sana kwa mwanafunzi kumsahau yule aliyemfundisha. Hili hujenga mahusiano na kumbukumbu nzuri kati yako na yule uliyemfundisha.
Huwezi kufahamu kesho utamkuta wapi yule uliyemfundisha na atakusaidia kwa njia gani. Hivyo kufundisha wengine hujenga kumbukumbu nzuri na ya kipekee.