Kilimo Cha Mpunga Tanzania

Kilimo cha Mpunga Tanzania ni Kilimo Kizuri sana na maarufu sana na pia mpunga ni moja wapo ya mazao yanayozalishwa kwa wingi barani Afrika.

Mchele huliwa na watu wa jamii mbali mbali duniani kote na ni nafaka ya pili kuzalishwa kwa wingi baada ya mahindi.

Mpunga unaweza kutumika kama zao la chakula na biashara.

Kilimo cha mpunga huendelea vizuri kama eneo lina mvua na maji ya kutosha pamoja na kuwa na watu wengi ili kuupa huduma mbalimbali kama vile kung’olea majani.

Jinsi Ya Kuchagua Mbegu Ya mpunga

Chagua mbegu bora, nzuri ambazo hazina dalili yoyote ya kuathirika na ugonjwa, zilizojaa vizuri na zenye afya.

Mfano wa aina za mbegu nzuri za mpunga ni;

  • Supa
  • Kahogo Red
  • Rufiji
  • Saro.

Matibu Ya Mbegu Kabla Kupanda Mpunga

Tibu mbegu kabla ya kuzipanda. Hii hufanya mbegu ziweze kuchipua vizuri na kuwa mimea mizuri. Njia zinazoweza kutumika kutibu mbegu ni kama:

Kusafisha mbegu kwa kutumia maji ya moto ambapo unaweka maji jikoni na kuyaacha yapate moto kiasi kisha weka mbegu kwenye mfuko wa pamba na tumbukiza kwenye maji.

Hakikisha joto halizidi wala kupungua na mfuko haufiki chini. Toa mfuko kutoka kwenye maji ya moto na hamishia kwenye maji safi ya baridi.

Sambaza mbegu kwenye karatasi kavu ili kupoa na kukauka.

Inashauriwa kutokuhifadhi mbegu zilizotibiwa na baadala yake zipandwe mara moja kwenye kitalu au shambani.

Njia hii huondoa vijidudu vinavyoweza kusababisha ugonjwa.

Kuloweka mbegu ili kuifanya ipate unyevu nyevu wa kutosha kuchipua, kupunguza muda wa kuanza kuota na kuzuia mbegu kuoza.

Wakati wa kuloweka badilisha maji ili kuondoa viini venye sumu na kuwezesha hewa safi kuingia.

Kabla ya kuchipuka Kausha mbegu na zifunike na majani kwa masaa 24 hadi 48.

Hii husaidia huhakikisha kuwa mbegu zinachipua kwa wakati mmoja, huzuia kuchipuka kuliko kithiri na huruhusu mzunguko wa hewa ambao unahitajika ili kuchipua.

Jinsi Ya Kuotesha Mpunga

  • Kwa kawaida gramu 80-100 za mbegu hupandwa kwenye mita 1 (80-100g/m2)
  • Tawanya/eneza mbegu kwa usawa katika kitalu
  • Usididimize kitalu baada ya kuotesha mbegu
  • Tumia kiasi cha mbegu angalau kilo 20 kwa ekari moja

Jinsi Ya Kutayarisha Kitalu

  • Lima angalau wiki mbili kabla ya kuotesha na kufurika.
  • Kandika/changanya tope angalau wiki moja kabla ya kuotesha na tengeneza kitalu kilichonyanyuka.
  • Ondoa maji kwenye kitalu siku moja kabla ya kuotesha ili kuimarisha sehemu ya juu ya udongo
  • Hakikisha udongo wa juu sio laini sana kwani itasababisha mbegu kuzama chini.
  • Mwagilia siku chache baada ya kuotesha ili udongo uwe na unyevu wa kutosha na hakikisha viwango cha kudidimia na maji havizidi agalau 1cm-3cm.
  • Siku moja kabla ya kung’oa na kupandikiza, ongeza kiwango cha maji kwenye kitalu kutoka 3 cm-10 cm ili kurahisisha ungo’aji na upandikizaji kwa kuondoa udongo ugandao kwenye mizizi.

Jinsi Ya Kutayarisha Shamba La Mpunga

inashauriwa kulima shamba lako na kufunika udongo angalau siku 15 kabla ya kupanda miche au mbegu moja kwa moja.

Hii husaidia kuulinda mche kutokana na vijidudu visababishavyo maradhi kutoka kwenye udongo pia huzuia kupotea kwa nitrogen.

Jinsi Ya Kupandikiza Miche Shambani

Ni muhimu kuondoa miche kutoka kwenye kitalu na kuipanda shambani mara tuu inapofikia ukubwa wa kutosha.

Miche inakuwa tayari kati ya wiki tatu hadi nne tangu kuotesha kutegemeana na mwanga wa jua, hali ya joto na aina ya mbegu.

Nafasi ni kati ya 20×10 au 20×20 (Mstari kwa mstari na mmea kwa mmea) kutokana na aina ya mbegu. Kina cha upandaji cha 3 cm kinashauriwa ili kuwezesha mizizi kuchipua na kushika vizuri.

Jinsi Ya Kupanda Mpunga Moja Kwa Moja

Njia hii imekuwa ikitumiwa na wakulima wengi kwa muda mrefu ambapo mbegu za mpunga hutawanywa shambani moja kwa moja.

Kazi za shambani hupungua kwa kiasi kikubwa lakini pia uzalishaji hupungua kutokana na kuwa na magugu mengi na ugumu wa kuhudumia mimea shambani.

Uharibifu na Magonjwa Ya Mpunga

Uharibifu wa mpunga hutokana na vijidudu, mimea au wadudu ambao wanauwezo wa kushusha kiwango cha uzalishaji wa mmea kwa mfano magugu, wadudu, panya buku na ndege.

Sababu za kufumuka kwa magonjwa au wadudu zinaweza kuchangiwa na utumiaji wa madawa ya kuulia wadudu na utumiaji wa mbolea (nitrogen) kwa kiwango kikubwa au kwa muda mrefu sana.

Wadudu kama vile viwavi wanaweza kuzuilika kwa kupanda matembo tembo kando kando ya shamba la mpunga na magugu kuzuilika kwa kupandikiza miche shambani badala ya kupanda mbegu moja kwa moja.

Jinsi Ya Kuvuna Mpunga

Kati ya miezi 4 hadi 6 (kutokana na aina) baada ya kupanda mpunga unakuwa umekomaa. Inashauriwa kuvuna katika muda muafaka ili kuzuia hasara itokanayo na wadudu, ndege na panya.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply