Tabia Zinazoleta Umasikini Kwenye Maisha

Mambo yanayo zuia mafanikio kwenye maisha Tanzania ni mengi sana na ukiwachunguza sana watu waliofanikiwa utagundua kuwa kuna tabia au mambo kadhaa yanayoshabihiana kati yao.

Pia ukiwachunguza watu walioshindwa au ambao hawajafanikiwa, utabaini pia kuna tabia au mambo kadhaa yanayofanana kati yao.

1. Masikini hawajali muda

Mafanikio yamefugwa kwenye muda. Ili mtu aweze kufanikiwa ni lazima ajifunze kutumia muda wake vyema. Watu wasiofanikiwa hawana mipaka; huchelewa kila mahali, pia hawathamini muda wa wengine.

Hawana vipaumbele wala muda wa kuweka malengo na vipaumbele kwenye maisha yao; wao huishi tu kulingana na lile linalokuja mbele yao.

2. Masikini wana visingizio

Walioshindwa hutoa visingizio vikubwa; husingizia na kulaumu kila kitu. Kila mara watu hawa hutafuta njia ya kuficha udhaifu wao kwa njia ya visingizio.

Watu waliofanikiwa nao wanakosea, lakini hujifunza kutokana na makosa yao na siyo kutengeneza visingizio.

3. Masikini hawana malengo

Malengo ni ramani muhimu ya kukuongoza kufika kwenye mafanikio au kutimiza ndoto zako. Watu walioshindwa hawana malengo wala hawafahamu faida za kujiwekea malengo maishani mwao.

4. Masikini hawachagui mwenzi sahihi wa maisha

Swala la mwenzi sahihi wa maisha linapuuzwa na watu wengi bila kufahamu umuhimu wake. Mwenzi sahihi kwenye maisha atakuwezesha kufanya mambo mbalimbali kama vile:

  • Kukusaidia kuweka na kutimiza malengo yako.
  • Kukushauri na kukutia moyo.
  • Kukusaidia katika mipango na mikakati ya kutimiza ndoto zako.
  • Kujali na kuheshimu hisia na utu wako.

Ni wazi kuwa watu waliofanikiwa wanafamu umuhimu wa kuwa na wenzi sahihi kwenye maisha. Unapokosa mwenzi sahihi utapata mwezi ambaye hana malengo wala maono; vipaumbele vyake ni matumizi na anasa.

5. Masikini hawafanyi matendo

Watu wengi ni wazungumzaji kuliko watendaji. Hili ni kinyume kwa watu waliofanikiwa kwani wao huweka kwenye matendo zaidi bila hata kujali kama watakwama au laa.

Ni muhimu kujifunza kuweka kwenye matendo mawazo na mipango yetu mbalimbali kuliko kuizungumzia pekee.

6. Masikini wanahirisha sana

“Nitafanya kesho”, “Bado kuna muda”, “Ni mapema sana kufanya hili”, “Bado najifikiria”, n.k. Ni baadhi ya kauli zinazopendwa na watu wanaopenda kuahirisha mambo.

Watu ambao hawatafanikiwa huahirisha kila jambo, huamini kuwa maisha yao yanajengwa kesho na si leo. Hili ni tofauti kwa watu waliofanikiwa kwani wao huamini kuwa maisha ya kesho huandaliwa leo.

7. Masikini hawawezi kusema hapana

Kila mara nimekuwa nikisisitiza kuwa jibu la hapana lina nguvu na umuhimu sana. Kusema hapana ni jambo linalofanywa sana na watu waliofanikiwa kuliko wale wasiofanikiwa.

Jibu la hapana humtenga mtu na mipango, watu, na hata vitu visivyokuwa na umuhimu kwenye maisha na malengo ya mtu husika.

Hivyo watu wasioweza kusema hapana, kamwe hawawezi kufanikiwa kwani huchukuliwa na kila mawimbi kisha hushindwa kufanikiwa.

8. Masikini hawapendi maarifa

Ni watu wachache sana ndiyo wanaofahamu umuhimu wa maarifa katika mchakato mzima wa kufanikiwa.

Watu waliofanikiwa hujifunza mambo mengi kadri wawezavyo ili kuongeza maarifa na uelewa wao. Maarifa sahihi na ya kiwango cha kutosha, yatakuwezesha kufanya maamuzi sahihi na bora kwenye maisha yako.

Ikiwa husomi vitabu, makala (mfano hii), kusikiliza na kutazama vipindi vinavyoongeza kiwango chako cha maarifa; kamwe huwezi kufanikiwa.

9. Masikini wana matumizi mabaya ya pesa

Hili ni janga linalowakabili watu wengi ambao bado hawajafanikiwa. Watu wengi hupata pesa lakini zinakwisha bila kujua wamefanya nini chenye manufaa kwao.

Ni muhimu kama mtu anapenda kufanikiwa akajifunza matumizi mazuri ya pesa. Hii itamwezesha kutumia pesa kuendeleza na kufikia ndoto zake.

10. Masikini wanawaza sana kushindwa

Maisha yetu ni matokeo ya vile tunavyofikiri. Ikiwa unafikiri kuwa huwezi, wewe ni maskini, hutofanikiwa n.k. Basi utakuwa hivyo.

Mara nyingi utasikia watu wakisema “mimi siwezi hili”, “huu ni udhaifu wangu”, “hili limeshanishinda”, “nikishindwa jambo nimeshindwa” n.k. Haya ni mawazo ya kujikwamisha wewe mwenyewe.

Ikiwa hutaacha mawazo haya, basi ni vigumu sana kufanikiwa kwani yatakuwa ni kizuizi kwako. Amini kila kitu kinawezekana; ni fikra zako tu ndiyo zinakukwamisha.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

2 Comments
  1. Nashukuru pia uko vizuri sana na naendelea kutekeleza nijitahidi nipate mafanikio japo kidogo

Leave a reply

Wauzaji
Logo