Tabia Zinazoleta Mafanikio Kwenye Maisha

Watu wengi hufikiri kuwa mafanikio kwenye maisha ni jambo linalotokea kwa bahati lakini mafanikio ni matokeo ya tabia au mikakati inayofanywa mara kwa mara.

1. Jitahidi Kuwa na Mipango

Watu waliofanikiwa hawafanyi kazi bila mipango madhubuti. Watu hawa hupanga mipango mbalimbali wanayotakiwa kuitekeleza na mwishoni hukagua kama mipango yao wameitekeleza jinsi ipasavyo.

Ni muhimu kujifunza tabia hii ya kujiwekea mipango na kufanya mambo kulingana na mipango husika bila kusahau kufanya tathimini mwishoni.

2. Jitahidi Kuacha Kuahirisha Mambo

Watu waliofanikiwa hawana tabia ya kuahirisha mambo, bali huyafanya kadri wapatapo muda. Mara nyingi watu wa kawaida hujidanganya kuwa kuna muda, kesho ipo au nitafanya baadaye.

Ikiwa tunataka kufanikiwa, ni lazima tufanye mambo bila visingizio wala kuahirisha.

3. Jitahidi Kufanya Kazi Kwa Bidii

Ni rahisi kufikiri kuwa watu waliofanikiwa wanalala au kukaa tu na pesa zinawajia. Watu waliofanikiwa wanajua nini maana ya kufanya kazi kwa bidii kweli.

Hakuna kitu kizuri kinachokuja kwa urahisi. Ni lazima kufanya bidii na kuwa na nidhamu ya kazi ndipo tunaweza kuona matokeo mazuri.

4. Jitahidi Kufanya Kitu Unachokipenda

Watu wengi waliofanikiwa wanafanya kile wanachokipenda ndiyo maana wanakifanya kwa bidii na kwa ufanisi mkubwa.

Ni muhimu kujifunza tabia hii ya kufanya kile unachokipenda kutoka kwa watu waliofanikiwa ili tuweze kufikia ndoto zetu.

5. Jitahidi Kuweka Malengo

Hakuna mtu yeyote aliyefanikiwa bila malengo chini ya jua. Malengo ni mwongozo wa wewe kufikia mafanikio yako.

Watu waliofanikiwa wamejenga tabia ya kujiwekea malengo stahiki pamoja na mikakati ya kuyatimiza. Kila mara wanahakikisha wanafanya jambo kufikia au kuendeleza lengo lao.

Ni muhimu kufahamu kuwa lengo ni matokeo ambayo mtu anataka kuyafikia katika kipindi fulani cha muda na hivyo ni muhimu kubainisha matokeo hayo pamoja na njia utakazotumia ili kuyafikia.

6. Jitahidi Kusoma Sana

Watu wengi hasa waafrika hawapendi kusoma. Watu husoma ikiwa kuna mitihani au kitu kingine cha lazima sana.

Watu waliofanikiwa wanasoma vitabu na makala nyingi kila mara kadri wanavyoweza. Mfano mzuri ni bilionea Bill Gates na Mark Zuckeberg, hawa wamekuwa mabalozi wakubwa wa vitabu pamoja na kuwahamasisha watu kusoma vitabu.

Kuna maarifa na hekima kubwa sana iliyofichwa kwenye vitabu; hivyo ni muhimu kujiwekea utaratibu wa kusoma vitabu na makala mbalimbali kama hii unayoisoma kutoka Fahamuhili.com.

Epuka kusoma vitu visivyo na tija kama vile udaku na maswala ya burudani.

7. Jitahidi Kuwa na Udhubutu

Watu wengi wana mawazo mazuri lakini wana hofu na wasiwasi wa kuyafanyia kazi mawazo yao. Hali hii ni kinyume kwa watu waliofanikiwa kwani wao hufanya juu chini ili kufanyia kazi mawazo yao.

Hawaogopi kushindwa wala kupata hasara. Hivyo ikiwa tunataka kufanikiwa, ni lazima tuwe na udhubutu na ujasiri wa kufanya mambo.

8. Jitahidi Kulinda Afya Yako

Afya njema ndiyo msingi wa mafanikio yetu. Kamwe hatuwezi kuzalisha au kufanya kazi yoyote yenye tija ikiwa hatutakuwa na afya njema.

Watu waliofanikiwa wamejijengea utamaduni wa kukagua afya zao pamoja na kufanya mambo mbalimbali ili kuzilinda.

Ni muhimu kuhakikisha tunafanya mazoezi, tunakula chakula bora pamoja na kufanya uchunguzi wa kitabibu kila tupatapo nafasi.

9. Jitahidi Kujali Muda

Kutokujali muda ni tatizo linalowakabili watu wengi. Kutokana na kukosa utaratibu mzuri wa kutekeleza majukumu, watu wengi hupoteza muda kwenye mambo ambayo hayana maana.

Watu waliofanikiwa wana ratiba iliyopangiliwa vizuri na wanayoifuata kila siku. Hawatawaliwi na mambo kama vile sherehe, mitandao ya kijamii, starehe, marafiki na michezo.

10. Jitahidi Kujenga Connection

Siri nyingine ya mafanikio inayofahamika vyema kwa watu waliofanikiwa, ni wanajua jinsi ya kujega connection (network) wa mahusiano na watu sahihi. Ili kukamilisha lengo au maono yako ni lazima utahitaji watu fulani kwa namna moja au nyingine.

Hivyo ni muhimu kujenga mtandao wa mahusiano na watu sahihi ambao watakuwezesha kwa njia moja au nyingine kufikia lengo lako.

Tuandikie Email Yako Uweze Kupata Post za Wauzaji wa Tanzania Kwa Haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo