Mambo Ya Kuzingatia Unapotengeneza Website Ya Biashara

Website nyingi zinatengenezwa kila siku Tanzania, lakini siyo zote zinakidhi viwango vya ubora na inasababishwa na website nyingi kutengenezwa bila kuzingatia kanuni muhimu za utengenezaji wa tovuti au blog.

Zipo athari nyingi za kutengeneza website yenye ubora mdogo kama vile kupoteza wasomaji au watembeleaji pamoja na kupata rank ya chini kwenye search engine.

1. Jitahidi Kuchagua Muundo Mzuri wa Website

Kosa la muundo mbaya wa website hufanywa na watu wengi sana, hasa kutokana na maarifa duni ya usanifu mtandao. Kwa mfano unakuta menu iko huku, ukurasa huu uko kule, tangazo limefunika maandishi, vitu vimejibana kwa pembeni.

Ni muhimu ukahakikisha website yako inasomeka vizuri na inavutia; ikiwa utatumia kiolezo (template) basi hakikisha unachagua kiolezo kizuri na cha kisasa

2. Jitahidi Kuchagua Mwandiko Unaosomeka

Mwandiko unaofaa kwako unaweza usifae kwa wasomaji wako. Hivyo kumbuka uwezo wa kuona na upendeleo wa miandiko hutofautiana baina ya mtu na mtu. Ni muhimu kuhakikisha mwandiko unaoutumia kwenye website au blog yako unasomeka vizuri kwa kila mtu.

3. Jitahidi Website Yako ifunguke Kwa Haraka

Kutokana na usanifu duni, matumizi ya teknolojia ya zamani au hata kuweka mambo mengi kupita kiasi katika ukurasa mmoja, kunafanya website nyingi kuwa na kasi ndogo ya kufunguka.

Unaweza kufanya haya yafuatayo:

  • Punguza picha, video au sauti zinazopunguza kasi ya kufunguka.
  • Tumia teknolojia za kisasa zinazowezesha website au blog kufunguka kwa kasi (Web compression and caching).
  • Punguza website za nje zinazofungukia ndani ya website yako kwa njia ya iframe.
  • Tumia webhost bora.

Kama utazingatia mambo haya, utaweza kuongeza watembeleaji zaidi kwani hakuna mtu anayependa kusubiri kusoma website inayochukua muda mrefu kufunguka.

4. Jitahidi Kuepuka Kulazimisha Usajili

Kamwe usifanye kosa la kumlazimisha msomaji au mtembeleaji kujisajili kwa lazima. Hakikisha unaandaa maudhui bora au unampa msomaji kitu chenye thamani kwake kitakachomfanya ajisajili mwenyewe.

Hakuna mtu atakayepoteza muda kujisajili kwenye website yako ikiwa anaweza kupata kitu anachokitaka kutoka kwenye website nyingine bila kujisajili na hivyo utapoteza kiasi kikubwa cha watembeleaji.

5. Jitahidi Kuchagua Kuepuka Video Zinazoanza Zenyewe

Hakuna kitu ninachokichukia kwenye website kama video au sauti zinazocheza zenyewe. Vitu hivi ni vibaya kwani vinamaliza data pamoja na kutoa maudhui ambayo mtembeleaji hayahitaji.

6. Jitahidi Kuepuka Matumizi Mabaya Ya Picha

Picha ni sehemu muhimu ya website au blog ikiwa zitatumiwa jinsi ipasavyo. Hakikisha unatumia picha zenye ubora stahiki, tena ambazo hazifunguki kwa tabu.

Epuka kutumia picha kubwa sana au za gif ikiwa hakuna ulazima; unaweza kutumia picha nzuri za ukubwa wa wastani ili usipunguze kasi ya kufunguka kwa website au blog yako.

7. Jitahidi Kuepuka Matangazo Yanayokera

Nani asiyependa kupata pesa kupitia blog? Naamini hakuna; ikiwa unapenda kuweka matangazo mbalimbali kwenye website au blog yako hakikisha matangazo husika hayamkeri mtumiaji.

Tumia matangazo machache na mazuri ambayo hayataingilia utendajikazi mzuri wa website au blog yako.

Kumbuka kuepuka matangazo yanayovamia browser ya mtumiaji na kufanya mambo mbalimbali bila ridhaa yake.

8. Jitahidi Kuweka Sehemu Ya Kusearch Vitu

Hakikisha kama unataka kutengeneza website au blog nzuri, huachi kuweka fomu ya kumuwezesha masomaji kutafuta vitu kwenye website au blog yako.

Hakikisha kila kilichoko kwenye website yako kinaweza kupatikana kupitia sehemu ya utafutaji (search field).

Kumbuka ikiwa mtembeleaji atahitaji kufahamu kama kitu fulani kiko kwenye website au blog yako atatumia fomu hii.

9. Jitahidi Kuweka Pages za Msingi

Kuna kurasa za msingi zinazopaswa kuwepo kwenye kila website au blog; kurasa hizo ni kama vile: Kutuhusu, Wasiliana nasi, Sera ya faragha au Vigezo na masharti.

Kurasa hizi zitamwezesha mtumiaji kufahamu kuhusu website au blog pamoja na wamiliki wake; pia zitamwezesha mtembeleaji kufahamu njia za kupata msaada au kuwasiliana na wahusika.

Si hayo tu, bali hata sheria na kanuni zinazotawala website husika zitaonekana vyema kwenye kurasa hizi.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha hupuuzi nafasi ya kurasa hizi. Kumbuka! Google hawawezi kutangaza kwenye website au blog ambazo hazina kurasa hizi.

10. Jitahidi Kuepuka Kumuunganisha Mtembeleaji Hovyo

Unahitaji watembeleaji wajiunge kwenye orodha yako ya barua pepe au vitaarifu? Kama jibu ni ndiyo, basi usiwaunge kwa lazima kwani wataichukulia website au blog yako kuwa inaingilia uhuru wao binafsi.

Hakikisha umempa mtembeleaji kitu chenye manufaa kitakachomfanya aone kuwa kuna umuhimu wakujiunga kwenye website au blog yako.

11. Epuka Kukusanya Taarifa za Mtumiaji Kwa Siri

Kukusanya taarifa za mtumiaji kwa siri bila ridhaa yake ni kosa kisheria ni lazima ufahamu sera na taratibu zinazotawala faragha ya mtumiaji.

Hivyo kuwa makini unapotaka kukusanya taarifa kama vile jina, barua pepe, umri, jinsia, aina ya kifaa alichotumia au anwani mtandao. Hakikisha mtumiaji wa website au blog yako anafahamu wazi aina ya taarifa unazokusanya pamoja na matumizi yake.

12. Jitahidi Kuepuka Uandishi Duni

Uandishi wa kwenye website siyo sawa na ule wa kwenye kitabu au andiko la chuo kikuu. Hivyo ni muhimu ukajifunza uandishi bora na rafiki kwa wasomaji pamoja na injini pekuzi (search engines). Unaweza kuhakikisha haya yafuatayo:

  • Aya na sentesi fupifupi.
  • Matumizi ya mishale na namba (kama ilivyotumika hapa)
  • Matumizi mazuri ya vichwa (H1-H6)
  • Matumizi mazuri ya viunganishi na maandiko pendekezwa.

13. Jitahidi Kuepuka Kuweka Links Zilizojificha

Inawezekana unataka kuweka kiunganishi mahali ambapo mtembeleaji wa website au blog yako atakibonyeza bila yeye kujua jambo hili ni baya kwani linakiuka kanuni za kuheshimu matakwa ya watembeleaji.

Hakikisha hufanyi kosa hili kwani hata search engine zinasisitiza kuepuka swala la kuficha links.

14. Jitahidi Kuzingatia Search Engine Optimization

Watu wengi wanaanzisha tu blog na website bila kujifunza wala kufahamu umuhimu wa uboreshaji wa injini pekuzi.

Uboreshaji wa injini pekuzi ni muhimu kwani utafanya website au blogu yako ionekane kwa watembeleaji. Hivyo hakikisha unafanya uboreshaji wa injini pekuzi jinsi ipasavyo.

Unaweza kuzingatia haya:

  • Chagua mada nzuri ya kuandika.
  • Epuka kunakili makala ua maudhui kutoka kwenye blog au website nyingine.
  • Andika kwa uandishi mzuri ambao unasomeka bila shida.
  • Tumia picha vizuri.
  • Andika makala au chapisho lenye urefu wa kutosha.
  • Weka taarifa za meta kwenye kila ukurasa (Maelezo ya ukurasa pamoja na kichwa.) Ikiwa unatumia WordPress unaweza kutumia Yoast SEO itakusaidia sana.

15. Jitahidi Kuepuka Maandishi Yanayochezacheza

Maandishi yanayochezacheza (blink) yamepitwa na wakati toka miaka ya 1990, hivyo kutumia maandishi haya hakumsaidii mtumiaji kwa njia yoyote bali humfanya aone website yako ni ya kizamani.

Kumbuka kuwa vivinjari mbalimbali havitambui tena mfumo wa maandishi haya.

16. Jitahidi Kuepuka Matumizi Teknolojia Ya Flash

Flash ni teknolojia ya kuweka video, picha, na sauti kwenye website. Kwa kiasi kikubwa ina changamoto nyingi na imeshapitwa na wakati.

Matumizi ya teknolojia ya flash hufanya website ifunguke kwa shida pamoja na kumuweka mtumiaji katika hatari ya kudukuliwa na wadukuzi wanaolenga teknolojia hii.

Inashauriwa kuepuka kutumia flash na badala yake utumie teknolojia ya HTML5

17. Jitahidi Kupangilia Vizuri Menu na Navigation

Mfumo wa viunganishi (menu) ni muhimu sana kwenye website yako, hivi humwezesha mtumiaji kuhama kutoka eneo moja la website au blog yako hadi lingine.

Ni vyema ukahakikisha mpangilio na mfumo wa viunganishi katika website yako umekaa vizuri na unaeleweka.

18. Jitahidi Kuchagua Matumizi Mazuri Ya Rangi

Watu wengi wana tatizo la kuchagua rangi hasa wanaume, hivyo ni vyema ukafahamu maana na ubora wa rangi kabla ya kuitumia kwenye website au blog yako.

Hebu fikiri blog au website yenye rangi nyekundu asilimia 98, je utaweza kuisoma vizuri? Naamini hutoweza; hivyo ni muhimu kuhakikisha unachagua rangi za website au blog yako kwa makini.

19. Jitahidi Kutumia Vizuri Javascript

Javascript ni lugha ya kompyuta inayotumika kutengenezea website; lugha hii hufanya kazi mbalimbali kama vile kufanya website kubadilika badilika kutokana na hali au tendo.

Javascript ni lugha muhimu katika utengenezaji wa website na blog, lakini ni muhimu ikatumiwa kwa kiasi na usahihi,

Kwani matumizi mabaya ya Javascript yataifanya website yako isifanye kazi vyema kwa watumiaji wengi. Kumbuka kuwa siyo vivinjari vyote vya watumiaji vitaweza kusoma lugha hii.

20. Jitahidi Kuepuka Matumizi Mabaya Ya Popup

Popup ni teknolojia ya kufungua vidirisha au viboksi ambavyo huingilia kati kile anachokifanya mtumiaji wa website husika.

Mara nyingi pop up humlazimisha mtumiaji kufanya kile kinachoonekana kwenye pop up kabla ya kuruhusiwa kuendelea na shughuli au lengo lake.

Matumizi ya pop up pamoja na madirisha mapya ya kivinjari huingilia matakwa au alengo la mtumiaji; hivyo humfanya aondoke kwenye website au blog yako kwani inaonekana kumvamia.

21. Jitahidi Kuepuka Kumlazimisha Mtembeleaji Kufanya Vitu

Ikiwa unalipwa kwa njia ya watembeleaji kubofya picha au kitu fulani kwenye website au blog yako, hakikisha huwalazimishi kufanya hivyo ili upate pesa.

Watembeleaji wakibaini hili hawatakuja tena kwenye website au blog yako kwani wataona kuwa unataka kuwatumia kuzalisha pesa na sio kuwapa kile wanachokihitaji.

22. Jitahidi Kuchagua Lengo La Website Mapema

Lengo ni muhimu sana kwenye kufanikisha jambo lolote. Website na blog nyingi hufa kutokana na kukosa lengo leo unaandika elimu, kesho siasa, keshokutwa habari, siku nyingine udaku au siku nyingine miziki,

Huku ni kukosa lengo na kwamwe hutoweza kufanikiwa kama hutoacha kosa hili la kukosa lengo. Bainisha unataka uandike nini, kwa ajili ya nani na kwa ajili ya nini.

23. Jitahidi Kuchagua Kuepuka Kumzuia Mtembeleaji

Nimeona baadhi ya watu wakifikiri kuwa kumzuia mtembeleaji kuondoka au kumlazimisha kukaa kwenye website au blog zao ndiyo kuzalisha faida zaidi.

Hakikisha mtembeleaji mwenyewe anaona sababu ya kuendelea kukaa kwenye website yako na si kwa kumlazimisha.

Ni kosa kuteka kivinjari au kifaa cha mtumiaji ili asiondoke kwenye website yako.

24. Jitahidi Kuzingatia Website Kama inafunguka Vizuri

Hivi leo asilimia kubwa ya watumiaji wa mtandao wanatumia simu za mkononi. Hivyo ni muhimu kuhakikisha website au blog yako inafunguka vyema kwenye vifaa vyote na si kompyuta pekee.

25. Jitahidi Kuepuka Kutumia Web Host Mbaya

Kuna mahali ambapo taarifa au maudhui ya website fulani hukaa eneo hili ndilo huitwa web host. Kutokana na ukosefu wa uelewa pamoja na kukwepa gharama watu wengi wamejikuta wakitumia host duni ambazo huathiri website zao kwa kiasi kikubwa.

Kumbuka host mbaya zina virusi, wadukuzi, hazipatikani wakati wote na zina kasi ndogo Unaweza kuzingatia mambo haya wakati wa kuchagua web host

  • Hakikisha inapatikana wakati wote (Uptime 99.9%)
  • Hakikisha inaulinzi madhubuti.
  • Hakikisha inahuduma nzuri kwa wateja (Saa 24).
  • Hakikisha wana huduma za kisasa na unazozihitaji.
  • Hakikisha wanaelezwa vyema na watumiaji wengine (Reviews).
  • Hakikisha gharama na njia zao za malipo zinaeleweka vyema.
Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply