
Vitu vya kuzingatia unapochagua bank ya biashara ni muhimu kufahamu kwasababu benki ni taasisi muhimu ambayo siyo rahisi mtu kukwepa kuitumia kwa njia moja au nyingine.
Kuhifadhi au kusafirisha pesa kwa njia za zamani kumepitwa na wakati sasa ni wakati wa kutumia mifumo salama na ya kisasa.
Kwa kuwa benki ni taasisi muhimu, huna budi kuchukua hatua kadhaa ili kupata benki nzuri kwa ajili ya shughuli zako za kifedha.
1. Jitahidi Kufahamu Usalama wa Pesa Zako
Kwa kawaida kila benki husimamiwa na benki kuu ya nchi ili kuhakikisha usalama wa fedha za wateja. Hata hivyo kuna baadhi ya benki huanzishwa na kuendeshwa kinyemela bila kuwa chini ya benki kuu.
Ni muhimu kuhakikisha benki unayotaka kuitumia imesajiliwa na inajiendesha kwa kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa taasisi za kifedha.
Unapotumia taasisi ambayo haijiendeshi kwa kufuata kanuni na sheria unaweza kupoteza pesa zako mara benki ipatapo matatizo kama vile kufilisika.
2. Jitahidi Kufahamu Gharama na Makato
Gharama na makato hutofautiana kati ya benki moja na nyingine. Ni muhimu ukafahamu gharama za makato kwenye benki husika ili uone kama unaweza kuyamudu.
Kwa mfano kuna benki hutoza shilingi 1500 kwa kutoa pesa kwenye ATM wakati nyingine hutoza shilingi 700. Hivyo chunguza gharama za kila huduma ili uone kama unazimudu.
3. Jitahidi Kufahamu Kuhusu Riba
Kwa kawaida benki nyingi hutoa riba na hutoza riba kwenye mikopo. Ni vyema ukachunguza viwango vya riba kwenye kila huduma ya benki husika ili uone kama unaridhika navyo.
4. Jitahidi Kufahamu Njia za Kuweka na Kutoa Pesa
Zama zimebadilika, maisha ya kwenda kuunga foleni benki siku nzima ili kutoa au kuweka pesa yamepitwa na wakati.
Benki nzuri na za kisasa zinatoa huduma mbalimbali kama vile kutoa au kuweka pesa kwa kupitia mawakala au simu za mkononi.
Ni muhimu ukachunguza kama benki unayotaka kuichagua ina huduma hizo na ni za uhakika.
5. Jitahidi Kufahamu Kuenea kwa benki
Kuna benki zina tawi moja au mawili nchi nzima. Kujiunga na benki kama hii kunaweza kukusababishia changamoto nyingi.
Hakikisha benki unayoichagua imeenea kwa kiwango cha kutosha hata ikibidi nje ya nchi ili usikose huduma za kifedha mara uwapo mahali popote.
6. Jitahidi Kufahamu Upatikanaji katika Mtandao
Kama nilivyotangulia kusema, mambo yamebadilika hivi leo pesa hazitumiki katika masoko au maduka ya kawaida pekee.
Unaweza kutuma na kupokea pesa kwenye mtandao wa intaneti, unaweza kununua na kuuza vitu kwenye intaneti au hata kuingia kwenye akaunti yako ya benki kwa kupitia mtandao.
Kwa kufahamu hili, ni muhimu kuhakikisha kama benki unayotaka kuichagua ina huduma za kibenki za kwenye mtandao ili usikwame mahali.
7. Jitahidi Kufahamu Huduma kwa wateja
Huduma nzuri na ya uhakika kwa wateja ni kiashiria kikubwa cha biashara au taasisi bora. Unapotumia benki unaweza kukutana na changamoto kadhaa au ukahitaji kufahamu mambo kadhaa.
Ni muhimu kuhakikisha huduma kwa wateja katika benki unayotaka kuichagua ni ya uhakika.
8. Jitahidi Kufahamu Huduma Zinazopatikana
Kila benki ina huduma zake au kwa lugha nyingine bidhaa zake inazotoa kwa wateja. Ni muhimu ukachagua benki ambayo ina huduma au bidhaa unazozihitaji na zenye manufaa kwako.
Chunguza maswala kama vile mikopo, bima, aina za akaunti, n.k. ili kuona kama zinakufaa na kukidhi mahitaji yako.
9. Jitahidi Kufahamu Upatikanaji wa Pesa
Ni rahisi kufikiri kuwa kila benki ina fedha za kutosha. Kuna baadhii ya benki zinajiendesha kwa kusuasua, unaweza kuhitaji kiasi fulani cha pesa lakini wakakuambia hawana kiasi hicho au usubiri wateja waweke pesa.
Sipendi kutaja mifano halisi hapa ili kulinda taswira ya benki hizo, lakini ukichunguza vyema utabaini kuwa zipo benki zenye mzunguko duni sana wa pesa. Hivyo ni muhimu kuhakikisha uwezo wa upatikanaji wa pesa katika benki unayotaka kuichagua.
10. Jitahidi Kupata Mrejesho wa Wateja Wengine
Wateja ndio wenye tathimini sahihi ya biashra au taasisi yoyote. Kabla ya kuchagua kutumia benki fulani, hakikisha wateja wa benki hiyo wanatoa mrejesho mzuri wa huduma wanazozipata.