
Vitu vya kuzingatia Kabla ya kufungua kampuni au kufungua biashara yako Tanzania ili uweze kupata mafanikio katika siku za mbeleni kwenye maisha yako.
1. Chagua wazo bora la biashara
Katika eneo ambalo watu wengi hukosea wakati wanapoanzisha kampuni au biashara ni uchaguzi wa wazo la kibiashara.
Unapochagua wazo baya au usilolimudu, ni wazi kuwa hutoweza kulitekeleza na kupata faida. Hakikisha wazo unalolichagua unalimudu vyema pia linatekelezeka.
Epuka kuchagua wazo pana sana au kuchagua wazo kwa sababu mwingine analifanya. Kwa kuwa wewe unaanza ni vyema ukachagua wazo unalolipenda, kulimudu vyema na linaloweza kukupa faida.
2. Fanya utafiti wa biashara
Kabla ya kuacha kazi yako au kile unachokifanya ili uanzishe kampuni yako, ni vyema ukafanya utafiti wa kina juu ya biashara utakayofanya.
Mambo ya kufanyia utafiti ni:
- Elewa biashara yako na huduma utakayotoa
- Fahamu wateja wako
- Fahamu ushindani
- Wafahamu watu utakaofanya nao kazi
- Fahamu njia bora ya mauzo ya bidhaa au huduma yako
3. Andaa business plan
Baada ya kufanya utafiti, sasa weka wazo au mpango wako katika karatasi. Mpango huu utakuwezesha kukuongoza katika kufikia malengo yako.
Kimsingi mpango wako wa biashara utajumuisha mambo kama vile:
- Mwonekano wa jumla wa kampuni
- Muundo wa utawala
- Ufafanuzi/Maelezo ya kampuni
- Malengo, Maono na mikakati
- Maelezo juu ya soko na tasnia unayoingia kufanya biashara
- Uendeshaji
- Mpango wa matumizi ya fedha
- Pamoja na taarifa nyingine za msingi zinazohusiana
4. Bainisha chanzo cha fedha
Ni lazima kubaini chanzo cha fedha utakazozitumia kuanzisha biashara au kampuni yako. Je fedha hizo zitatokana na mkopo, akiba yako au msaada?
Kumbuka uendeshaji wa kampuni unahitaji fedha kwa ajili ya shughuli mbalimbali kama vile matumizi ya ofisi, usafiri, malipo ya huduma na mishahara.
Ni vyema kulishughulikia hili mapema ili usije ukakwama katika biashara yako.
5. Tambua muundo wa biashara
Unatakiwa kubainisha muundo wa biashara au kampuni yako kabla hujaianzisha. Je kampuni au biashara yako itakuwa ni ya shirika, ubia au binafsi?
Unapochagua muundo zingatia yafuatayo:
- Ugumu wa uendeshaji kwa kila mfumo.
- Gharama za uendeshaji.
- Kodi.
- Sheria na vibali.
- Manufaa ya muundo husika.
- Mtaji.
Unapozingatia haya hakika utaweza kuchagua muundo wa kampuni au biashara wenye tija zaidi kwako.
6. Tafuta ofisi ya biashara
Watu wengi wamekuwa wakianzisha kampuni kwa mazoea bila kuzingatia kuwa ofisi ni muhimu kwa biashara au kampuni zao.
Tafuta ofisi utakayo mudu gharama zake, pia yenye kukidhi mahitaji ya kampuni au biashara yako.
Kama utaamua kufanyia kazi nyumbani, basi hakikisha unatenganisha mambo binafsi na yale ya ofisini. Kumbuka kuepuka kuchagua ofisi ya kifahari au ya gharama kubwa bila sababu ya msingi.
7. Changanua changamoto za biashara
Changamoto zipo kila mahali hivyo yakupasa kuzifikiria kabla ya kuanza kampuni au biashara yako. Kama unajidanganya kuwa utafanya biashara bila kukutana na changamoto yoyote unajidanganya.
Jitahidi uzitambue changamoto mapema ili uweze kuweka mikakati mapema ya namna utakavyo pambana nazo.
Nashukuru Sana Kwa elimu yenu ila ninaomba utupe hata mfano wa kuandaa business plan maana wengine hatujui jinsi ya kuandaa.
Asante sana Daniel kwa comment yako na nimefurahi sana kuiona.
Pia kuhusu swala la kuandika business plan ukiangalia kwa makini kwenye post zangu za nyuma utaliona pia.