Mambo Ya Kuzingatia Kabla Ya Kuanza Biashara

Kuanza biashara kutoka kiwango cha sifuri siyo kazi rahisi ni muhimu kufahamu vitiu vya kuzingatia kabla ya kuanza biashara na jinsi ya kupambana na changamoto.

Hivi ndivyo wajasiriamali wengi wanavyojifunza na kukua. Unapokuwa kwenye biashara ni lazima ufahamu makosa ambayo yanaweza kuathiri biashara au uwekezaji wako ili ujitahidi kuyaepuka ama kuyapunguza kadri iwezekanavyo.

1. Jitahidi Kuepuka Kujifanya Unajua Kila Kitu

Usijifanye unajua kila kitu, hasa kama ndiyo umeingia kwenye ulimwengu wa kibiashara. Kwanini? Kwa sababu kuendesha biashara ni kujifunza na kupata uzoefu.

Jitahidi kujifunza na kujijengea uzoefu kupitia maarifa mbalimbali ili uweze kuendesha biashara yako vyema kama mjasiriamali.

2. Jitahidi Kuepuka Kuanza Biashara Bila Miundombinu

Ni dhahiri kuwa wengi husema “mwanzo ni mgumu” lakini ni lazima utengeneze miundombinu kadhaa. Unapoanzisha biashara kama mjasiriamali jitahidi kuweka miundombinu kadhaa ya muhimu kwanza kabla hujaanza kufanya biashara.

Kuendesha biashara kunahitaji vifaa na rasilimali kadha wa kadha ambazo ni muhimu ziandaliwe kabla. Miundombinu hii inaweza kuhusisha mtaji, vifaa muhimu au ofisi ndogo ya kuanzia Kumbuka hivi ni vile vitu vya msingi tu na siyo mbwembwe zisizokuwa na msingi.

3. Jitahidi Kuepuka Kuchagua Mshirika Asiyefaa

Awali ya yote, siyo lazima kuanza biashara kwa ushirika wa mtu mwingine. Kama umejiandaa vyema unaweza kumudu kusimamia na kuendesha biashara yako vyema bila tatizo.

Lakini kama unahisi ni muhimu kuwa na mshirika basi chagua mshirika ambaye mnaendana kifikra. Huyu atakuwezesha na kukuunga mkono na kukusaidia kutimiza malengo na maono yako.

Lakini ukichagua mshirika siyefaa ni dhahiri atakuzamisha.

4. Jitahidi Kuepuka Kutazama Mafanikio Pekee

Biashara yako au mradi hauwezi kukua ikiwa mipango yako haibadiliki na Wewe kama mjasiriamali unatakiwa ufikiri kwa upana unapokuwa unafanya maamuzi.

Kutazama tu mafanikio bila kuzingatia ubora wa huduma ni kujizamisha majini wewe mwenyewe. Ni dhahiri kuwa kuzingatia kumudu kuwa na ubora wa huduma pamoja na ukuaji wa biashara ni jambo zuri zaidi.

5. Jitahidi Wateja Wakutafute

Je ni kweli kuwa unataka wateja wakutafute na wakati soko limejaa wajasiriamali wengine na huduma? Hapana! Kama unataka kukuza msingi wako wa wateja ni lazima uwe pale ambapo wateja wapo.

Kwa kufanya hivi watakutambua na kununua huduma au bidhaa yako.

6. Jitahidi Kuepuka Kupuuza Nafasi Ya Teknolojia

Wajasiriamali wengi wa Kiafrika wanadhani kuwa teknolojia ni kwa ajili ya wazungu au kampuni kubwa. Haijalishi ni biashara au mradi gani unaoufanya ni lazima uzingatie nafasi ya teknolojia.

Teknolojia iko kila mahali; hivyo ni vyema ukatumia teknolojia kama vile intaneti kutangaza, kuuza, na hata kuwasiliana na wateja wako.

7. Jitahidi Kuepuka Matumizi Mabaya Ya Fedha

Watu wengi hawana matumizi mazuri ya fedha hasa wao binafsi. Tatizo hili limekuwa pia likijitokeza pale mtu anapotakiwa kusimamia na kutunza pesa za mradi au biashara.

Wengi huishia kuzitumia kwenye mambo yao binafsi au kwa mambo ambayo hayana tija kwa kampuni au mradi.

Ni lazima uwe na nidhamu ya pesa kama mjasiriamali ili uweze kuiwezesha biashara yako kukua; tambua hii ni pesa ya mradi au biashara na si ya matumizi yangu binafsi.

8. Jitahidi Kuepuka Kujipanua Bila Mpangilio

Wajasiriamali wengi huwa wana mawazo makubwa na mazuri lakini wanakosa mikakati na mipango mizuri ya kuitekeleza.

Unafungua mradi fulani leo na unafanikiwa ndani ya muda mfupi, nawe bila hata kujenga msingi imara wa kiuchumi na rasilimali nyingine unakimbilia kufungua mwingine au tawi.

Hili ni kosa ambalo limeua maduka mengi yanayoanzishwa na wajasiriamali. Jifunze kujiandaa na kuweka misingi imara pale unapotaka kupanua au kuongeza mradi wako ili ule wa awali usife.

9. Jitahidi Kuepuka Kuajiri Wafanyakazi Wasio na Uwezo

Kama ni lazima kuajiri watu basi epuka kosa hili ambalo mara nyingi wajasiriamali hulifanya kwa huogopa garama za kuajiri watu wenye uwezo kwa ajili ya kufanya nao kazi.

Ni dhahiri kuwa “rahisi inaumiza”; hivyo ni vyema ukaajiri hata mtu mmoja bora kuliko kuajiri watano wenye uwezo duni.

Ukizingatia hili utajikuta unapata matokeo stahiki kutoka na kile ulichowekeza.

10. Jitahidi Kuepuka Kupuuza Maoni Ya Wateja

“Mteja ni mfalme”; je unalifahamu hili? Wajasiriamali wengi hupuuzia maoni ya wateja bila kujua kuwa maoni ya wateja ndiyo huwawezesha kujirekebisha na kuweza kuwapa wateja wao kile wanachokihitaji.

Kosa hili lisiposhughulikiwa litakupotezea kiasi kikubwa cha wateja na kuleta matokeo mabaya kwenye biashara au mradi wako.

11. Jitahidi Kuepuka Kuacha Fursa Zikupite

Wajasiriamali wengi hupenda kungojea mazingira yawe mazuri bila hata kujali fursa zinazopotea. Ni dhahiri kuwa hakuna mtu atakaye kutengenezea mazingira unayotaka ukiona fursa itumie na mambo yatakaa vyema mbele ya safari.

Inawezekana fursa unayoiona leo kesho isiwepo tena.

12. Jitahidi Kuepuka Kukataa Ushauri wa Kitaalamu

Kila kitu kizuri kinahitaji maarifa stahiki ili kiweze kutokea Ni dhahiri kuwa wajasiriamali wengi wanafanya kosa la kupuuza ushauri wa kitaalamu katika kazi zao kwa kuona kuwa hauna nafasi.

Kwa mfano kama unafuga kuku au unalima mazao fulani kwanini usimwite mtaalamu wa kilimo au mifugo ili akushauri? Ni dhahiri kuwa ukipata ushauri wa kitaalamu utakuwa mwenye tija zaidi.

13. Jitahidi Kuepuka Kutokwenda na Soko

Mjasiriamali mzuri ni yule anayefahamu kuwa kwa sasa soko linataka nini. Ni lazima uweze kuepuka kosa la kutokutazama mahitaji ya soko, ili uhakikishe mauzo ya bidhaa au huduma yako hayaathiriki.

Kwa mfano zamani watu walinunua zaidi kuku walio hai, lakini leo soko la kuku waliochinjwa ni kubwa pia; kwanini wewe bado unauza tu kuku walio hai?

Ni dhahiri ukitazama mfano huu utaona jinsi kosa hili linavyowaathiri wajasiriamali wengi katika maeneo mbalimbali.

14. Jitahidi Kuepuka Kushindwa Kubaini Wateja Lengwa

Ni lazima wewe kama mjasiriamali uwabaini wateja wako ili huduma au bidhaa yako iuzike.

Kwa mfano umetengeneza dawa ya kuua mbu, kisha unaiuza mikoa ya baridi badala ya mikoa yenye joto (kwenye mbu wengi); ni dhahiri kuwa hutoweza kupata wateja wa bidhaa yako sawa sawa.

Chukua hatua leo na uwafuate wateja sahihi wa huduma au mradi unaoufanya.

15. Jitahidi Kuepuka Mbinu Duni za Masoko

Maswala ya masoko ni taaluma kamili ambayo watu hujifunza katika shule na vyuo mbalimbali. Hivyo ni muhimu wewe kama mjasiriamali kutokupuuzia taaluma hii kwani ndiyo itakayokuwezesha kubaini njia bora na sahihi za kuuza huduma au bidhaa yako.

Hakikisha mbinu za masoko unazifahamu vyema tena zinaendana na soko husika la bidhaa yako. Hakikisha pia mbinu zako zinabadilika kulingana na mazingira na hali ya soko.

Tuandikie Email Yako Uweze Kupata Post za Wauzaji wa Tanzania Kwa Haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo