Kilimo Bora Cha Nyanya Na Soko La Nyanya Tanzania

Kilimo cha Nyanya Tanzania Hufanywa kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi ya tanzania Pia Nyanya ni miongoni mwa mazao jamii ya mboga mboga.

Tunda la nyanya hutumika kama kiungo muhimu katika mapishi na utengenezaji wa kachumbari na pia kama tunda.

Faida za Kilimo cha Nyanya

Nyanya ni chanzo kizuri cha vitamini mwilini na hutengeneza kipato kizuri kwa mkulima kama zikilimwa vizuri kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo na uzalishaji Pia Nyanya huhitajika zikiwa mbichi au zikiwa zimesindikwa

Nyanya hutumika kutengeneza bidhaa nyinginezo kama vile nyanya za kopo na tomato sauce. na pia Nyanya ni mmea wa sehemu za joto na hukua vizuri kwenye viwango vya joto baina nyuzi 18 hadi 24º Sentigredi.

Mmea wa nyanya hunawiri kwenye udongo unaopitisha maji vizuri.

Udongo Unaofaa Kwenye Kilimo cha Nyanya

Udongo unaonata haufai kwa kilimo cha nyanya kwani unahitaji umwagiaji wa maji wa hali ya juu. Udongo lazima ukaguliwe kama una chumvi au boroni nyingi au ukosefu wa madini mengineo.

Mazao mazuri hupatikana kwenye udongo wenye uchachu (pH) wa 6.5. Uwe na mfumo wa kubadili mazao katika eneo kila mara ili kupunguza magugu, maradhi na ongezeko la wadudu.

Nyanya hupendelea udongo unaopitisha maji kwa urahisi na wenye rutuba ya kutosha na hivyo hupenda Udongo uwe umetifuliwa vya kutosha au matuta kuruhusu mizizi kushika vema.

Hali ya Hewa inayofaa kwa Kilimo cha Nyanya

Kwa kawaida nyanya huhitaji hali ya hewa iliyotulia na kavu ili kuweza kufanya vizuri. Lakini nyanya humudu mazingira mengi.

Mazingira yenye baridi kali au joto kali huharibu ukuaji pamoja na uzaaji wa nyanya. Udongo wowote wenye virutubisho hai unafaa kupandia nyanya kinachotakiwa ni kuhakikisha kuwa udongo unaweza kuupa mmea chakula kiasi kinachohitajika kukua na kuzaa. 

Matumizi ya maji yanatakiwa yaangiliwe vizuri ili kuhakikisha kuwa maji hayazidi wala kupungua kwani maji mengi husababisha mizizi kuoza, ni chanzo cha magonjwa na mmea kudumaa.

Aina za Udongo

Kuna aina kuu tatu za udongo

• Kichanga (Sand soil) una uwezo mdogo wa kuhifadhi maji na unyevunyevu. Hivyo, hukauka upesi.

• Tifutifu (Loam soil) unahifadhi maji vizuri na upatikanaji wa maji na virutubisho kwa mimea ni mkubwa.

• Mfinyanzi (Clay soil) unahifadhi maji mengi zaidi, bali upatikanaji wa virutubisho kwa mimea ni mdogo.

Vipimo vinavyoonyesha hali ya rotuba ya udongo ni

• Tindikali ya udongo

• Kiasi cha mboji

•Kiasi cha Naitrojeni, Fosfati, Potashi, Salfa, Chokaa (Calcium) na Magnesium. Vilevile kiasi cha zinki, shaba, manganese na boroni vinapimwa. Kipimo cha PH ya udongo (Soil pH)

PH ni kipimo kinachoonyesha kiwango cha tindikali au nyongo katika udongo. Udongo waweza kuwa na tindikali (ph ndogo kuliko 7), nyongo (ph kubwa kuliko 7), au katikati (neutral) – ph ya 7.

Tindikali au nyongo ya udongo hupimwa kwa kutumia pH mita. Mazao mengi hustawi zaidi katika udongo wenye hali ya tindikali ya wastani (kipimo cha pH 5.5 hadi 7.0).

Aina za Zao La Nyanya

Kuna aina kuu mbili za nyanya kulingana na ukuaji wa mmea

 • Nyanya ndevu (mfano Money maker)
 • Nyanya fupi zenye kutoa matawi mengi mfano Roma, Tanya na Cal J.

Aina ya mbegu za nyanya

 • Kawaida (opv variety)
 • Chotara (Hybrid F1)

Kiasi Cha Mbegu za Nyanya Kwenye Kilimo cha Nyanya

Kwa ekari moja utahitaji Mbegu gram 100-150 kwa OPV variety, na Gram 30-50 kwa hybrid (F1) . Gharama za kutosha ekari moja kwa OPV variety ni tsh 100,000-180,000, na kwa Hybrid (F1) Gharama ni kati ya tsh 200,000-400,000 kutegemea na aina yenyewe ya mbegu na hekari.

Vipimo kati ya mimea wa nyanya na mistari ni Sentimita 90 X 90

 • Kupanda miche kwa karibu huleta mkusanyiko mkubwa wa majani, jambo linalochangia kuzuka kwa maradhi na kupunguza nguvu za dawa za kupuliza.
 • Kwa zao nzuri na matunda bora ya nyanya tumia kipimo cha gramu 30 ya mbegu kwa ekari ili kufikia miche 9,000.
 • Nyanya uathirika na kiwango kidogo cha unyevu nyevu. Maji ni muhimu wakati wa kutoa maua na kuanza kupatika kwa tunda. Ukosefu wa maji kwenye kilimo cha nyanya kunaweza kuliua tunda.

Ukuzaji wa Miche Bora Ya Nyanya

Miche ya zao la nyanya huzalishwa kwenye kitalu kwa kupanda mbegu. Mbegu za nyanya huota baada ya siku 5 hadi 10. Baada ya kukua kitaluni kwa muda wa wiki 4 hadi 5 toka kuota kwa mbegu, miche hupandwa shambani.

Kabla ya kupandikiza shambani miche ya nyanya huandaliwa kwa kupunguza umwagiliaji maji kwa siku moja au mbili ili miche izoee hali ngumu kabla ya kuhamishiwa shambani.

Hapo shambani miche hupandikizwa kwa kuzamishwa katika kina kirefu zaidi ya ilivyo kuwa kitaluni.

Hii inasaidia miche kutoa mizizi ya pembeni mingi zaidi kwa ajili ya kufyonza maji pamoja na virutubisho aridhini.

Baada ya kupandikiza mwagilia maji yakutosha.

Usimwagilie maji juu ya mche wa nyanya. Katika kipindi cha jua kali, tandaza nyasi kwenye tuta ili kupunguza upotevu wa maji na unaweza kuweka kivuli kwa kutumia majani ya miti au migomba.

Kulingana na aina ya nyanya na rutuba ya udongo, nafasi ya kupandia ni sm 60 kati ya mstari hadi mstari na 45 hadi 60 nafasi ya mche hadi mche AU sm 90 kwa 50 AU 75 Kwa 40. 

Kama udongo hauna rutuba ya kutosha inapendekezwa kutumia nafasi kubwa ya kupanda.
Utunzaji wa zao la nyanya Nyanya fupi zisizo refuka kwenda juu, ni rahisi sana kutunza na
hazihitaji huduma nyingi.

Tatizo kubwa ni kuwa kwa kutambaa chini, katika kipindi cha mvua huwa karibu na magonjwa yatokanayo na udongo.

Katika kipindi cha jua kali, matunda huungua kwani mmea huwa na majani machache tu yanayo kinga matunda yasipigwe na mionzi ya jua.

Mbolea Kwenye Kilimo cha Nyanya

Licha ya mbolea ya kupandia, unashauriwa kuongeza mbolea kipindi cha wiki mbili au tatu baada ya kupandikiza miche bustanini. Mbolea hii ya kukuzia iwekwe kuzunguka shina la mmea kwa umbali wa sentimeta 5 hadi saba kutoka kwenye shina.

Kwa mbolea kama vile CAN, NPK, au SA tumia kifuniko kimoja cha maji ya uhai kwa shina. Mbolea hii inaweza kuwekwa mara mbili kabla ya mvuno wa kwanza wa nyanya. 

Ili kurefusha kupindi cha uzaaji wa zao la nyanya (na hata mazao mengine  yatoayo matunda kama vile nyanya chungu, biringanya, pilipili hoho, nk) inapaswa kuongezea mbolea katika kipindi cha uvunaji mfano baada ya kuvuna mara mbili unashauriwa kuongeza mbolea ya samadi na mbolea kama vile NPK.

Hii inasaidia mmea kuendelea kutoa maua bila kuchoka. Kwa kawaida nyanya fupi jamii ya “Roma” huweza kuzaa nakuvunwa kwa kipindi cha wiki 6 hadi 8 tu.

Lakini kama utakuwa unaongezea mbolea na kukazania matunzo ya bustani (hasa usafi wa bustani na kumwagilia maji ya kutosha), nyanya zinaweza kuendelea kuzaa kwa muda mrefu zaidi.

Hii ni tofauti na mazoea ya wakulima wengi kuwa mara nyanya zianzapo kuzaa huduma za palizi na usafi wa shamba huachwa na kutilia maanani kazi ya kuvuna pekee.

Hii inajitokeza zaidi kwenye aina ya nyanya fupi. Kwa nyanya fupi ni vizuri kuhakikisha kuna matawi mengi iwezekanavyo ili kuweza kupata matunda mengi zaidi.

Hivyo usipunguze matawi katika aina hii ya nyanya. Kwa nyanya ndefu zenye kuhitaji egemezi tunashauriwa kukuza nyanya kwa tawi moja lisilo na vichipukizi pembeni au matawi mawili na kuacha mnyanya urefuke.

Kupunguza majani ni muhimu pia katika kupunguza maambukizo ya ukungu katika shina na pia kutoa nafasi ili mwanga kupenya na kuruhusu mzunguko wa hewa.

Majani ya punguzwe kipindi cha asubuhi kwa kutumia mkono na siyo kisu kwani kinaweza kueneza magonjwa kutoka mche hadi mche.

Kwa nyanya ndefu majani ya chini ya matunda huondolewa kadiri unavyo endelea kuvuna.

Unashauriwa upunguze majani ya nyanya wakati wa asubuhi kwa kutumia mkono na pia usitoe zaidi ya majani matatu katika mmea kwa mara moja.

Namna Ya kupandikiza Miche kwenye Kilimo Cha Nyanya

 •  Panga kupandikiza miche shambani au bustanini siku ambayo jua siyo kali sana au wakati wa jioni wakati jua linakaribia kuzama.
 • Manyunyu ya mvua ni muhimu na husaidia sana wakati wa kupandikiza.

Chotara (Hybrid F1) Chotara (Hybrid F1) Chotara (Hybrid F1)  Shindilia udongo vizuri kuzunguka mizizi ya mche kwa kutumia vidole vyako ili kuufanya mche ujishike vizuri kwenye udongo.

 • Hakikisha unaweka nafasi ya kutosha kati ya mmea na mmea na mstari hadi mstari ili kuacha nafasi ya mizizi kutanukia na majani kuchanulia hapo baadaye.
 • Kama hamna mvua wakati wa kupandikiza inashauriwa kumwagilia hata kama mimea haionyeshi dalili za kukauka.
 •  Ikinge mimea iliyopandikizwa na jua la moja kwa moja hadi wakati ambapo itaonyesha kuwa imeshika kwenye udongo, inaweza kukua yenyewe na kuhimili mwanga wa jua. 

Umwagiliaji wa Kilimo Cha Nyanya

Nyanya ni zao linalohitaji maji mengi sana kwa ajili ya ukuaji wammea na matunda yake. Umwagiliaji uwe wa kulingana kwa kila siku iliyo pangwa.

Usibadilishe ovyo kiasi cha maji na ratiba ya kumwagilia. Hii inasababisha kuoza kwa kitako cha nyanya. Pia ili kutunza maji katika udongo, inashauriwa kuweka matandazo katika mzunguko wa shina la nyanya au bustani yote.

Hivyo katika umwagiliaji ni busara kuzingatia kiasi hiki cha maji katika kipindi kama hiki. Pia kama unatumia keni, mpira au bomba usimwagilie maji juu ya matawi ya nyanya kwani umwagiliaji wa namna hii utasababisha kuenea kwa magonjwa ya ukungu.

Magonjwa Katika Kilimo Cha Nyanya

 1. Bakajani chelewa (Late blight)

Ugonjwa huu huenenzwa na vimelea vya fangasi. Husababishwa na hali ya hewa haswa ya unyevunyevu, na huenezwa na upepo. Majani, shina, matunda nyanya hushambuliwa.

Majani huwa na ukungu mweupe na kijivu, na baadaye hukauka. Matunda huwa na mabaka ya kikahawia na baadaye kuoza. Mashina pia huwa na mabaka ya kikahawia.

Jinsi Ya Kudhibiti
 • Nyunyiza dawa ya kuzuia ukungu hasa wakati wa masika, Dawa zinazopendekezwa ni Ridomil, Dithane 45, Bravo, Funguran, milraz.
 • Fanya mzunguko wa mazao. Usipande nyanya sehemu moja kila msimu au
 • palipolimwa mazao jamii ya nyanya km viazi mviringo, bilinganya, aina zote
 • za pilipili na nyanya chungu.
 •  Tumia mbegu safi Panda aina za nyanya zinazovumilia ugomjwa

2. Bakajani tangulia (Early blight)

Huenezwa na vimelea vya fangas Pia Husababishwa na kuenezwa na hali ya hewa pamoja na mbegu zenye ugonjwa.

Mabaka ya kahawia yenye mistari ya mviringo huonekana kwenye majani na shina Pia Baka jeusi hutokea sehemu ya tunda inayoshikana na kikonyo.

Jinsi Ya Kudhibiti
 • Nyunyiza dawa ya Kocide, Funguran
 • Teketeza mabaka ya mazao baada ya kuvuna
 • Tumia mbegu safi na bora

3. Mnyauko fusari (Fusarium wilt)

Huenezwa na mbegu zenye ugonjwa. Husambazwa na vimelea vya fungasi vinavyoishi kwenye udongo. Ugonjwa hujitokeza zaidi wakati wa kiangazi.

Vimelea hushambulia sehemu au mirija ya mmea ya kupitishia maji na chakula. Mmea hukosa maji na chakula na hatimaye hunyauka.

Shina la mmea likipasuliwa ndani huonekana rangi ya kikahawia.

Udhibiti wake
 • Tumia mbegu safi na bora
 • Tumia mzunguko wa mazao. Nyanya zisizungushwe na mazao jamii yake
 • Teketeza masalia ya mimea
 • Choma kitalu cha nyanya kabla ya kusia mbegu

4. Mnyauko bacteria (Bacterial wilt)

Ugonjwa husababishwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye udongo. kupitishia maji na chakula hushambulia na mimea hunyauka ghafla.

Mmea wa nyanya hukauka na kufa. Huenezwa na kusambazwa na mbegu na udongo wenye vimelea.

Udhibiti
 • Panda mbegu safi
 • Panda nyanya sehemu ambayo haijawahi kupandwa viazi mviringo, bilinganya au nyanya chungu
 • Tumia mzunguko wa mazao
 • Hakikisha mfereji wa maji ya kumwagilia hayapiti kwenye shamba lenye historia ya ugonjwa huu.
 • Choma kitalu cha nyanya kabla ya kusia mbegu

5. Mnyauko vetisili (Verticillum wilt)

Hakuna dawa inayozuia au kutibu ugonjwa huu kwa sasa. Ugonjwa husababishwa na ukungu (fangasi) kwenye udongo. Ukungu huu huishi kwenye udongo kwa muda mrefu bila kudhurika na Ugonjwa huongezeka ikiwa mizizi ya nyanya imeshambuliwa na minyoo fundo au kukiwepo na hali ya ubaridi au ukame.

Ugonjwa huu wa nyanya husababisha hasara kubwa pia Ugonjwa hushambulia sehemu ya ndani ya shina nakusababisha sehemu hiyo kuwa na rangi ya kijivu na Majani hugeuka njano na mimea hunyauka na kufa. 

Udhibiti
 • Tumia mzunguko wa mazao usiopungua miaka mine
 • Ondoa mabaki ya nyanya shambani
 • Tumia mbegu bora na safi za nyanya

6. Bakadoa (Bacterial spot)

Ugonjwa huu huenezwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye mbegu pia kwenye hewa. na Huenezwa kwa kasi sana wakati wa masika. Madoa ya rangi ya kahawia huonekana kwenye majani na matunda.

Udhibiti

· Panda mbegu bora na safi za nyanya

· Tumia mzunguko wa mazao

· Teketeza masalia ya mazao ya nyanya

· Nyunyizia dawa ya funguran, Kocide101, Cobox, Bravo

7. Makovu bakteria (Bacterial canker)

Ugonjwa huu wa nyanya huenezwa na vimelea vya bacteria vinavyoishi kwenye mbegu na hewani. Hutokea zaidi wakati wa masika.

Majani hukauka nchani na makovu yaliyodidimia hutokea kwenye shina. Matunda ya nyanya huwa na makovu yenye rangi ya kahawia sehemu ya katikati.

Udhibiti

· Tumia mbegu bora na safi za nyanya

· Teketeza masalia ya mazao ya nyanya

· Tumia mzunguko wa mazao

8. Rasta (Yellow leaf curl)

Ugonjwa huu husababishwa na virusi na huenezwa na nzi wadogo weupe. Hutokea zaidi wakati wa kiangazi. Mimea hudumaa na majani yaliyoshambuliwa huwa na rangi ya manjano na pengine rangi ya zambarau pia Nyanya hupasuka.

Udhibiti

· Nyunyiza dawa za sumu za kuua wadudu (Selecron, Dursburn, Actelic)

· Ng’oa mimea ya nyanya yenye ugonjwa

· Tumia mzunguko wa mazao

· Weka shamba la nyanya katika hali ya usafi

9. Batobato (Tomato mosaic virus)

Ugonjwa husababishwa na virusi na huenezwa na mbegu kwa kugusana. Majani huwa na mchanganyiko wa rangi hasa kijani kibichi na kijani kilichofifia (manjano).

Majani hujikunja na majani machanga huwa na maumbile yasiyo kawaida.

Udhibiti

· Tumia mbegu za nyanya bora na safi

· Ng’oa mimea ya nyanya iliyoshambuliwa

· Teketeza masalia ya mazao ya nyanya

· Weka shamba la nyanya katika hali ya usafi

Wadudu Wanao shambulia Nyanya

 1. Viwavi Matunda (Fruit worm)

Viwavi hawa hutokana na wadudu nondo. Viwavi hutoboa matunda ya nyanya na kuacha matundu na hatimaye matunda huoza pia Hupunguza ubora wa nyanya.

Udhibiti

Nyunyizia dawa ya kuua wadudu. Dawa hizo ni pamoja na Actelic 50EC, Selectron, Dursbaan, Maji ya majani ya mwarobaini au utupa pia huua wadudu.

2. Utitiri wekundu (Red Spider mites)

Hawa ni wadudu wekundu, wadogo sana wanaoweka utando chini ya majani, hasa wakati wa kiangazi. Wadudu hawa hufyonza utomvu kwenye majani na kusababisha majani kukauka.

Udhibiti

· Nyunyizia dawa za sumu. Dawa hizo ni pamoja na Actellic, Selecron, Dursbarn na Thionex

· Mwagilia maji mara kwa mara

· Weka shamba katika hali ya usafi

3. Inzi weupe (White flies)

Hawa ni Inzi weupe wadogo sana. Hujitokeza sana wakati wa kiangazi Hueneza ugonjwa wa virusi ujulikanao kama Rasta.

Udhibiti

Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Selecron, Actellic, Dursban nathionex. Pia maji ya majani ya mwarobaini na utupa.

4. Vidukari au Wadudu mafuta (Aphids)

Ni wadudu wenye rangi nyeusi au kuijani au kahawia. Hukaa chini ya majani na kufyonza utomvu kwenye majani machanga. Hudumaza mmea wa nyanya na kushindwa kuzaa matunda

Udhibiti

Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban maji ya majani ya mwarobaini na utupa, maji ya pilipili.

 5. Minyoo (Nematodes)

Ni minyoo midogomidogo ambayo hushambulia mizizi na kuweka vifundo. Mizizi hushindwa kuchukua maji na chakula kwenye udongo. Mimea hudumaa na kushindwa kuzaa

Udhibiti

· Tumia mzunguko wa mazao

· Choma udongo wa kitalu kabla ya kusia mbegu kwa kutumia karatasi la plastiki jeusi na nishati ya jua

· Choma masalia ya mazao ya nyanya kwa sababu Hushambulia miche ya nyanya hasa baada ya kupandikizwa shambani. Wakati wamchana hujificha kwenye udongo

6. Sota (Cutworms)

usiku hujitokeza na kukata miche kwenye shina usawa wa udongo.

Udhibiti

· Nyunyiza dawa za kuua wadudu kwenye shina usawa wa udongo

· Hakikisha miche inapata maji ya kutosha.

Upungufu wa virutubisho aina ya chokaa. 
Dalili zake ni matunda ya nyanya kuoza sehemu ya kitako na kuonyesha rangi nyeusi. Kuzuia ugonjwa huu, zingatia kuwa na utaratibu mzuri wa kumwagilia maji ambao haubadiliki ovyo kiratiba na kiasi cha maji
yanayowekwa.

Rutubisha mimea ya nyanya kwa madini ya chokaa kwa kutumia mbolea aina ya CAN zenye madini haya.

7. Ugonjwa wa ukoma wa nyanya
Huu ni ugonjwa wa virus unao enezwa na inzi mweupe. Inzi hawa hushambulia zaidi nyanya wa kati wa kiangazi, hasa kipindi cha joto kali.

Dalili

• Majani machanga ya nyanya hujikunja na baadaye majani yote.
• Kupungua kwa utoaji maua na matunda na hata yakitokea matunda huwa ni madogo.
• Mmea kudumaa na kutozaa kabisa.

Mbinu za Kuzuia ni kupunguza kuenea kwa ugonjwa huu wa nyanya kwenye shamba kwa kudhibiti kuzaana na kuenea kwa mdudu (inzi mweupe)

• Kuondoa mimea michache ya nyanya iliyo shikwa na ugonjwa maana wadudu hawa wanachukua ugonjwa huu kutoka mimea hii.
• Kutumia mbegu zilizo hakikishwa kuwa zinaweza kuvumilia ugonjwa huu na kutoa mavuno mazuri.
• Usilime nyanya karibu na eneo lililo na mazao kama bamia, mipapai kwasababu mimea hii Uhifadhi inzi mweupe.
• Kuua inzi weupe wanaofyonza nyanya na kusambaza virusi kwa kutumia madawa. Tumia madawa kama vile Selecron, Decis, Karate n.k.
• Epuka kuchanganya zao la nyanya na mazao mengine yanayohifadhi hawa nzi kama vile mipapai na bamia.
• Ng’oa na kuchoma moto mimea yote iliyougua ugonjwa huu.

Ratiba ya mbolea katika kilimo cha zao la nyanya na kuzibiti wadudu na magonjwa

Hatua ya kwanza

 • NPK 15.9.20 +TE(yaramila winner) Gramu 10 kupanda bila kuweka samadi
 • Yara mila winner Gram 5 pamoja na samadi kwa shina / shina moja
 • Tenganisha kwa kuweka tabaka la udongo usio na mbolea kwa sentimita mbili kati ya mbengu na udongo uliyochanywa na mbolea
 • Epuka mbegu kugusana na mbolea inaweza kuungua na kushindwa kuota
Hatua ya pili (A) Kuweka mbolea ya kukuzia katika udongo
 • Weka mbolea ya kukuzia ya NITROBAR wiki tatu baada ya mche kuota  au mche wenye majani matatu(3)baada ya utokaji
 • Weka mbolea ya ujazo wa kifuniko cha soda / kijiko kimoja kidogo cha chai sawa na gramu tano katika kila shina la mche mmoja
 • Weka mbolea kwa umbali wa kiasi cha sentimita 5 kutoka mzunguko wa shina alafu fukia zingatia kuweka mbolea hii mapema kabla ya kutoa maua
Hatua ya pili (B) Kuweka mbolea  ya kukuzia  kupitia majani (Busta)
 • Tracel Bz/NPK+TE foliar+supergro –pulizia mbolea hii kwa miche ya nyanya ikiwa na majani matatu hadi manne ya kuchipua
 • Changanya Tracel BZ maganda matatu ya kibiriti katika maji ya lita 15 puliza juu ya majani ya mche
 • Rudia tena baada ya siku kumi na nne (14) zingatia kutumia mbolea hii kabla ya maua kutoka
 • Mbolea hii ni mtiririko wa mbolea ya kukuzia sambamba na nitrobar izingatie kutumia kabla ya maua
Hatua ya tatu kuweka mbolea ya uzalishaji wa matunda

Maua na matunda ya nyanya yatakapotunga wiki ya sita na nane weka tena npk 15.9.20+ TE(yaramila winner) gram 10 kwa shina (kijiko cha chakula)

Weka mbolea umbali wa nchi 6 mzunguko wa shina unaweza kuongeza gram 5 hadi 10 baada ya siku ya 21 kama kuna viashirio vya upungufu wa rutuba shambani kwa kuangalia ubora matunda na muonekano wa majani ya nyanya

Matumizi ya madawa ya wadudu na magonjwa

Siku moja kabla ya kupanda pulizia dawa eneo la kupandia kwa kutumia dawa moja kati ya hizi Duduall, farmerguld, biotren au dawa inayolingana na hizi.

Tumia moja wapo tumia dawa hizi na dawa ya kavu (fungicide) kama megasin M au jamii yake changanya dawa hizi mbili pamoja (iwapo zitakubali kuchanganyika kwa kufuata vipimo katika kifungashio pulizia mils 30 hadi 50 katika shimo la kupandia kabla ya kuweka mbegu

Kuzibiti aphids na wadudu wengine kwenye kilimo Cha nyanya

Baada ya utoaji wa majani mawili hadi matatu tumia dawa ya nyanya yenye kiambata cha imidacropid kama farm guard pamoja na DUDU-ACELAMECTIN nk

Kwa mchanganyiko wa pulizia farm guard 8-15 mls/20l na DUDU-ACELAMECTIN 20-30mls/20l  katika majani ya mimea wa nyanya na shina lake kwa kulainisha udongo ili dawa ifike katika mizizi na kunyonywa na mmea Rudia tena baada ya siku 14 hadi 21

Kudhibiti magonjwa na wadudu katika kilimo cha nyanya

Tumia dawa za magonjwa aina ya super grino au ivory m72 au redomil gold gram 50 hadi 70 katika maji ya lita 15  pulizia miche yenye majani manne Rudia tena kila siku kumi hadi 14.

Tumia Dimethiate kudhibiti inzi wa watunda yanapokuwa makubwa  hadi kuvuna.

Kuzibiti magonjwa mbalimbali ya nyanya

Kipindi cha kutoka maua na matunda tumia megasini na supergrino matumizi changanya megain M Gram 50 vijiko vidogo 10 maji lita 15 pulizia kila siku 14 kwa kupishana na supergrino kwa mtiririko wa siku saba pulizia megasin M

Wiki inayofuata supergrino iwapo kutakuwa na tishio la mabaka meusi  katika matunda dawa ya copper oxychloride (tankopa) itatumika kila siku 14

Ushauri huu unaweza kubadillishwa kulingana na kubadilika kwa Teknolojia ya kilimo, mazingira ya mazao yanapoliwa, taarifa ya vipimo vya udongo au aina tofauti tofauti za wadudu na magonjwa yaliyojitokeza

Jinsi ya kumzibiti mdudu tuta absoluta (Kanitangaze)

Kuna madawa mengi (AMAMECTIN BENZOATE) ambayo yanatoa matokeo mazuri ukiyatumia lakini changamoto imekuwa ni bei na usugu ambao mdudu huyu anautengeneza.

Dawa ambazo mpaka sasa zimetoa matokeo mazuri juu ya mdudu huyu wa kanitangaze ni Amsac, Crotale, cutter, wiltigo, Virtako, Ampligo, tank mix ya match na dynamec, pegasus, trigard, belt, couragen, runners and evisect.

Unapokuwa unatumia dawa hizi jaribu kuzichanganya wakati wa upigaji kwa mfano ukipuliza pegasus mara nne sitisha kuitumia tena tumia virtako hii itasaidia wadudu kutotengeneza usugu.

Usitumia dawa za jamii moja kwa kufuatana hapa namaanisha dawa zenye kufanana mode of action. Katika dawa nilizotaja hapo juu isipokuwa evisect zingine zimeonesha matokeo mazuri kwenye funza ili hali evisect imeonyesha matokeo mazuri kwenye vipepeo.

Kupambana na mdudu kanitangaze inatakiwa IPM means Integrated Pest Management ifatwe. Katika IPM itakupasa kuwa na lures ambazo hutoa harufu ikavutia madume ya tuta wanapokuja unakuwa unetegesha kwenye beseni la maji wanakufa hii itasaidia kupunguza uzalianaji wa tuta kwa sababu madume watakuwa wachache.

Lakini pia kuna lure nyingine ya kupuliza asubuhi sana hii huwafanya funza wote kuja juu ya majani hapa ukipiga dawa matokeo ni asilimia mia ya kumuua huyu mdudu.

Njia nyingine ya kumdhibiti ni kulima kwenye green house ama agronets ila hapa inahitaji umakini mkubwa akiingia madhara yake huwa makubwa na kwa muda mfupi.

Tuta absoluta anaweza teketeza shamba kwa muda mfupi sana kwa sasa ukienda sokoni nyanya nyingi utakuta zina alama nyeusi ama matundu hayo ni madhara ya mdudu anaeitwa kanitangaze.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

8 Comments
 1. Nimejifunza mengi sana kutoka kwenu kuhusu kilimo cha nyanya, Asante kwa elimu nzuri

 2. Asante nimejifunza zaidi kilimo bora cha nyanya na soko lake inshallah

 3. Asante kwa elimu nzuri ya kilimo cha nyanya yaani nimepata faida kubwa ya kufahamu mambo mengi sana juu kilimo hiki

 4. Elimu yenu ya kilimo cha nyanya kwakweli ni nzuri sana Mungu awabariki.

Leave a reply