Kilimo Bora Cha Bamia Tanzania

Kilimo cha bamia ni maarufu sana kwa Tanzania na Bamia ni zao la mbogamboga linalotambulika kitaalamu kama Abelmoschus esculentus lenye asili ya Ethiopia na Afrika ya magharibi.

Kwa sasa kilimo hiki kinalimwa katika nchi nyingi hasa sehemu za joto. Baadhi ya maeneo yanayolima kilimo cha bamia kwa Tanzania ni pamoja na mikoa ya Morogoro, Dodoma, Tabora, Pwani na Mbeya.

Matumizi Ya Bamia

Kilimo cha bamia hulimwa kwa ajili ya matunda yake ambayo hutumika kama mboga au kiungo katika mapishi mbalimbali majumbani.

Vilevile katika nchi zilizoendelea nyuzi nyuzi zinazotokana na bamia hutumika katika utengenezaji wa karatasi.

Aina za Mbegu za Bamia

Kuna aina tofauti za mbegu za bamia zinazopatikana Tanzania kama vile Clemson Spineless, Emerald Green, White Velvet, Perkins Mammoth na Dwarf Prolific.

Mbegu za Bamia

 1. Clemson spineless Mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa mita 1 hadi 1.5 na kuzaa bamia za kijani zenye urefu karibu cm 15 na Huchukua siku 55 hadi 58 kuanza kuvuna.
 1. Emerald green Mbegu hizi za bamia zina tabia ya kukua hadi urefu wa m 1.5 na kuzaa bamia za kijani zenye urefu wa cm 18 hadi 20 na Huchukua siku 58 hadi 60 kuanza kuvuna.
 1. White velvet Mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa m 1.5 hadi 1.8 na kuzaa bamia ndefu, nyembamba, zilizochongoka na zenye urefu wa cm 15 hadi 18.

Uchaguzi wa Eneo La Kulima Bamia

Ni muhimu kuchagua eneo linalofaa kwa kilimo cha bamia kabla ya kuanza uzalishaji. Ni vyema eneo litakalotumika katika kilimo cha bamia liwe na urahisi wa upatikanaji maji kurahisisha umwagiliaji kwa kilimo cha umwagiliaji.

Vilevile shamba la bamia liwe lenye kufikika kwa urahisi ili kufanya wepesi katika kuhudumia shamba na usafirishaji wa mazao kwenda sokoni au kufikiwa kwa urahisi na wanunuzi wanaofuata mazao shambani.

Zao la bamia hushambuliwa sana na minyoo fundo (nematodes). Hivyo usichague eneo ambalo limetoka kutumika katika kilimo cha mazao yanayoweza  kushambuliwa na minyoo fundo kama vile viazi vitamu, nyanya, bilinganya na pilipili hoho.

Kwa tahadhari unaweza kulima zao hili katika eneo ambalo limetoka kutumika kwa kilimo cha mazao ya nafaka kama vile mahindi na mtama kwa kuwa mazao haya hayashambuliwi na minyoo fundo.

Eneo zuri Kwa Kilimo cha Bamia

Hali Ya Hewa na Mwinuko

Bamia ni zao linalopendelea hali ya joto hivyo hustawi katika maeneo yenye hali joto kuanzia nyuzi joto za sentigredi 21 hadi 35.

Ustawi mzuri zaidi huonekana katika maeneo yenye joto la nyuzi za sentigredi 21 mpaka 30 pia Hali joto zaidi ya nyuzi za sentigredi 42 huweza kusababisha kudondoka kwa maua.

Bamia hustawi vizuri katika maeneo ya mwinuko tofauti hadi mita 1000 kutoka usawa wa bahari yenye mvua za wastani.

Udongo Mzuri wa Kilimo

Kilimo cha bamia hustawi katika udongo wa aina nyingi wenye rutuba, kina, uwezo wa kuifadhi maji vizuri na usiotuamisha maji.

Hata hivyo zao la bamia hufanya vizuri zaidi linapolimwa katika udongo wa tifutifu yenye kichanga wenye rutuba ya kutosha na tindikali kuanzia Ph 5.8 hadi 6.5.

Mbegu za bamia hushindwa kuota kabisa pale joto la udongo linapokuwa chini ya nyuzi za sentigredi 16. 

Jinsi Ya Kuandaa Shamba La Bamia

 1. Muda wa Kuandaa

Shamba la bamia liandaliwe mapema mwezi mmoja kabla ya kupanda ili kuruhusu magugu na mabaki ya mazao kuoza vizuri.

Kwa kilimo cha bamia kwa kutegemea mvua ni vyema maandalizi yaanze mapema kabla ya kuanza kwa mvua za masika. Inashauriwa kuanza maandalizi mapema mwezi Januari.

Kwa kilimo cha  umwagiliaji unaweza kuanza maandalizi muda wowote kulingana na mahitaji na soko unalolilenga.

 1. Namna ya Kuandaa

Shamba la bamia huandaliwa kwa kufyeka nyasi, kung’oa visiki na kulima kabla ya kupima na kuweka matuta.

Kulima Shamba hulimwa kwa kutumia jembe la mkono, jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers au matrekta.

Matumizi ya jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers na matrekta hurahisisha shughuli ya kulima na kuifanya iwe na ufanisi kwani hukatua udongo vizuri na kuufanya uwe tifutifu.

Unapotumia jembe la mkono katika kulima hakikisha unakatua udongo katika kina cha kutosha sm 20 mpaka sm 30 na kulainisha mabonge.

Udongo uliokatuliwa vizuri hupitisha hewa inayohitajika na mmea, hurahisisha ukuaji wa mizizi na kuifadhi maji vizuri.

 1. Kupima shamba (field layout)

Ni muhimu kuanza kupima shamba la bamia kabla ya kuanza kuandaa matuta ili kupata matuta yaliyo katika mpangilio mzuri na mistari ya mimea shambani iliyonyooka vizuri.

Kabla ya kupima matuta ni muhimu pia kujua nafasi ya kupandia utakayo tumia ili kupata ukubwa sahihi wa kila tuta.

Kwa mfano kwa nafasi ya kupandia ya cm 60 × cm 40 kwa matuta makubwa unaweza kutengeneza kila tuta katika upana wa sm 1.2 na urefu wowote.  Acha nafasi ya m 1 kuzunguka shamba na njia kila baada ya tuta upana wa sm 50.

Tumia Tape measure au kamba yenye vipimo kupima shamba huku ukiweka alama za matuta na njia kwa kuchomeka mambo (pegs) katika kila kona ya tuta na kuzungushia kamba.

 1. Kuweka matuta

Inashauliwa kupanda bamia katika matuta ili kusaidia mizizi kukua vizuri na udongo kuhifadhi maji na wakati wa kiangazi tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo ili kufanya maji yaweze kukaa kwenye udongo

Wakati wa masika matuta ya bamia yainuliwe kidogo toka kwenye usawa wa ardhi ili kuzuia maji yasituame. Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa ya mkulima.

Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo hupandwa mstari mmoja. Tengeneza matuta ya kilimo cha bamia kwa kufuata alama zilizowekwa wakati wa kupima shamba.

Jinsi Ya Kupanda Bamia

Zao la bamia huweza kupandwa moja kwa moja shambani au kwa kuanzia kitaluni. Hata hivyo wakulima wengi hupendelea zaidi kupanda zao hili moja kwa moja shambani pasipo kupitia kitaluni.

Katika eneo lenye udongo mzito wenye asili ya mfinyanzi mbegu hupata shida kuota hivyo ni muhimu kuanzia kitaluni ili kuweza kupata miche mingi shambani.

Kwa kuanzia kitaluni hakikisha unafuata taratibu zote za uandaaji na matunzo ya kitalu cha mbogamboga na pandikiza miche pindi inapokua na majani halisi matatu hadi manne.

Maandalizi Ya Mbegu za Bami

Mbegu za bamia ni ngumu kidogo katika kuota hivyo ni vyema ziandaliwe ili kurahisisha uotaji wake. Mbegu za bamia huandaliwa kwa kuziloweka katika maji ya vuguvugu kwa muda wa masaa ishirini na nne ili kuchochea uotaji.

Mbegu za bamia huchukua muda wa siku 5 hadi 10 kuota. Kutegemeana na nafasi ya kupandia na uotaji wa mbegu kiasi cha kilo moja na nusu hadi kilo mbili na nusu za mbegu kinaweza kutosha kupanda katika eneo la ekari moja.

Nafasi Ya Kupandia Bamia

Bamia huweza kupandwa katika nafasi tofauti kuanzia sm 60 hadi 80 kati ya mstari na mstari na sm 30 hadi 50 kutoka shimo hadi shimo.Hakikisha unafuata maelekezo ya mbegu husika juu ya nafasi pendekezwa.

Hatua za Upandaji wa Bamia

 1. Mwagia maji mengi shambani masaa kumi na mbili kabla ya kupanda mbegu ili kulainisha udongo na kurahisisha upanzi.
 1. Chimba mashimo ya kupandia bamia yenye kina cha sm 2 hadi 3 katika nafasi iliyopendekezwa kwa mbegu itakayotumika mistari miwili miwili kila tuta kwa kutumia kamba iliyowekwa vipimo.
 1. Weka viganja viwili vya mkono vya samadi iliyoiva katika shimo la kupandia bamia kisha changanya na udongo kupata mchanganyiko mzuri.
 1. Kwa mbolea ya kupandia kama DAP weka nusu kizibo cha soda katika kila shimo la kupandia kisha fukia mbolea kwa tabaka dogo la udongo kabla ya kupanda mbegu za bamia. Kiasi cha kilo hamsini za mbolea ya DAP kinatosha kutumika katika  eneo la ekari moja.
 1. Panda mbegu mbili za bamia katika kila shimo, fukia kwa udongo mwepesi, shindilia na kisha mwagia maji.

Jinsi Ya Kutunza Shamba La Bamia

Matunzo ya shamba la bamia ni muhimu sana kwa sababu huamua kiasi cha mavuno unayoweza kupata kutoka shambani.

Shamba la bamia ambalo halipati matunzo mazuri hata kama mbegu bora inayozaa sana itatumika mavuno bado yatakuwa hafifu.

Umwagiliaji wa Shamba la Bamia

Njia za Umwagiliaji wa Bamia

Kuna njia tofauti za umwagiliaji wa bamia ambazo zinaweza kutumika katika umwagiliaji wa bustani ya bamia kama vile umwagiliaji wa njia ya matone (drip irrigation), wa njia ya mifereji na umwagiliaji wa kutumia cane.

Kwa kilimo cha kiangazi au pale mvua zinapokuwa hafifu ni muhimu kufanya umwagiliaji wa bustani yako ili kuepuka kunyauka kwa mazao shambani kutokana na upotevu mkubwa wa maji. Wakati wa kumwagilia hakikisha haumwagii maji katika majani bali katika shimo chini ya kichaka cha mche (canopy).

Ratiba Ya Umwagiliaji wa Bamia

Unaweza kumwagilia bustani ya bamia kila baada siku mbili hadi tatu kutegemeana na hali ya hewa na udongo.

Cha msingi usiache udongo ukauke bali mwagia maji angalau asilimia hamsini ya unyevu wa udongo unapokuwa umepotea.

Mambo Ya Kuzingatia Katika Umwagiliaji

Ni vyema umwagiliaji wa bustani uzingatie hatua za ukuaji wa mimea bustanini, hali ya hewa na uwezo wa udongo kutunza maji.

Mahitaji ya maji kwa zao la bamia huongezeka wakati wa kutoa maua na kutengeneza matunda. Vilevile katika maeneo yenye hali ya joto na udongo wa kichanga maji hupotea kwa urahisi.

Hakikisha maji hayatuami katika shamba lako kuepuka kuoza kwa mizizi na udongo haukauki.

Jinsi Ya Kupunguza Miche Ya Bamia

Ng’olea miche ya bamia katika shamba wakati wa kufanya palizi ya kwanza wiki nne tangu kupanda ikiwa na urefu wa sm 10 hadi 15. 

Bakiza mmea mmoja wenye afya katika kila shimo. Mimea iliyong’olewa kutoka katika shimo moja inaweza kupandikizwa katika shimo lingine ambalo mbegu hazikuota.

Jinsi Ya Kuweka Mbolea Kwenye Bamia

Weka mbolea ya kukuzia aina ya Urea wiki sita tangu kupanda kwa kiwango cha nusu kizibo cha soda kuzunguka shina sm 5 kutoka shina lilipo na kurudia kuweka tena kila baada ya wiki mbili hadi mwisho wa kuvuna.

Mmea wa bamia unapokuwa mkubwa wenye majani mengi usiweke mbolea ya kukuzia hadi bamia zitakapo toka vinginevyo mmea unaweza kuwa na majani mengi na kuzaa bamia chache. Mfuko mmoja wa Urea wa kilo 50 unatosha kutumika katika eneo la ekari moja.

Aina za Dawa za Kupiga Kwenye Bamia

 1. Dawa za ukungu

Uchaguzi wa dawa za ukungu hufuatana na magonjwa yanayoshambulia zao husika hivyo ni vema kujua magonjwa yanayoshambulia zao la bamia kabla ya kuchagua dawa za kutumia kama kinga au tiba pale magonjwa yanapojitokeza. 

Unaweza kuanza kupiga dawa ya ukungu wiki moja hadi mbili tangu miche ya bamia kuota na kurudia kila baada ya wiki moja hadi mbili kutegemeana na maelekezo ya dawa husika.

 1. Dawa za kuua wadudu

Nyunyizia dawa ya kuua wadudu baada ya kuona wadudu waharibifu katika shamba lako la bamia ili kuweza kuchagua dawa sahihi ya kudhibiti aina ya wadudu waliovamia bustani yako.

Jinsi Ya Kupalilia Shamba La Bamia

Palizi ifanyike kuanzia wiki ya nne tangu kupanda na kurudia kila baada wiki mbii hadi tatu. Hakikisha hakuna magugu bustanini katika kipindi cha kutoka maua na kutengenezwa kwa matunda.

Unaweza kupalilia kwa kutumia mikono, jembe dogo la mkono au dawa za viuagugu zinazopatikana katika maduka ya pembejeo za kilimo. 

Fuata ushauri wa wataalamu walio katika eneo lako na maelezo ya dawa kama yalivyo kwenye lebo ya chupa.

Jinsi Ya Kuweka Matandazo

Matandazo husaidia kudhibiti magugu, kuifadhi unyevu na kuongeza rutuba katika udongo. Kwa matokeo mazuri katika udhibiti wa magugu inashauriwa kuweka matandazo kwa kuyatandaza katika udongo katika kina cha sm 10 mpaka 15 maeneo yote ya tuta kuzunguka mashimo ya miche.

Matandazo ya asili kama mabua ya nafaka, pumba za mpunga, maganda ya karanga na maranda ya mbao yanaweza kuwekwa kabla ya kupandikiza baada ya kuchimba mashimo ya kupandia au baada ya kupandikiza.

Jinsi Ya Kuvuna Bamia

 1. Kiwango cha mavuno Ya Bamia

Kiwango cha mavuno ya bamia kwa ekari moja hutegemeana na matunzo ya shamba, uwezo wa kuzaa wa mbegu iliyotumika na idadi ya mimea katika shamba.

Mbegu za aina tofauti zina uwezo tofauti wa kuzaa na hivyo mavuno huwa tofauti. Vilevile mashamba tofauti yaliyopandwa mbegu ya aina moja na kupata matunzo ya viwango tofauti huwa na kiwango tofauti cha mavuno.

Kwa bustani ya bamia iliyopandwa mbegu bora na kutunzwa vizuri huweza kutoa mavuno wastani wa tani 5 hadi 8 kwa ekari.

 1. Muda wa Kuvuna Bamia

Bamia huchukua siku 50 hadi 60 kuanza kuvuna. Huwa tayari kuvunwa siku tano tangu kutoka kwa maua zikiwa bado changa na zenye urefu wa sm 5 hadi 10 kutegemeana na aina ya mbegu.

Hivyo basi inashauriwa kuvuna bamia kila baada ya siku tatu tangu mvuno wa kwanza wakati wa asubuhi. Uvunaji wa bamia unaweza kuendelea kwa muda wa siku 30 hadi 40 tangu mvuno wa kwanza.

 1. Mambo ya kuzingatia Katika Uvunaji

Usiache bamia zikomae kabla ya kuvuna kwa sababu bamia zilizokomaa huwa ngumu na zenye nyuzi nyuzi na hivyo hazina soko kwa matumizi ya nyumbani.

Vilevile kuacha bamia zikomae katika mmea husababisha mmea kuacha kuzaa mapema na hivyo mavuno huwa madogo.

Tumia kisu au mkasi wakati wa kuvuna ili kuepuka kuathiri shina na kusumbua mizizi ya mmea. Vilevile usivune bamia zinazoonyesha dalili ya kuoza au kuathiriwa na wadudu.

Kwa baadhi ya watu bamia huweza kusababisha muwasho wa ngozi hivyo hakikisha unavaa suruali ndefu na shati la mikono mirefu wakati wa kuvuna.

Hatua za uvunaji wa Bamia

 1. Andaa vifaa na vyombo vya kuvunia kama vile kisu, mkasi na ndoo au chombo chochote cha plastiki kwa kuvisafisha kwa maji safi na sabuni.
 1. Andaa sehemu utakayokuwa unaweka bamia wakati wa kuvuna iliyo kivulini karibu na shamba na utandike turubai.
 1. Wakati wa kuvuna kata kikonyo cha bamia karibu na tawi linaloshikilia tunda kisha weka tunda kwenye ndoo. Hakikisha unavuna bamia na kikonyo chake ili zisiharibike kwa urahisi.
 1. Ndoo inapojaa bamia beba ukazitandaze katika turubai lililo tandikwa karibu na bustani ili zipate hewa na zipoe kutoka katika joto la shamba (field heat) kabla ya kuzipakia.
 1. Safisha vizuri vyombo vya kuvunia kwa maji safi na sabuni kila baada ya kumaliza siku ya kuvuna ili kuzuia vimelea vya magonjwa.

Matunzo Baada Ya Kuvuna Bamia

 1. Jinsi Ya Kupakia Bamia

Baada ya kuvuna pakia bamia kwenye matenga au makreti yaliyo tengenezwa kwa mbao au plastiki yenye matundu yanayo pitisha hewa vizuri. Hakikisha upakiaji unafanyika kivulini ili bamia zisiunguzwe na jua.

 1. Jinsi Ya Kuhifadhi Bamia

Bamia huweza kuifadhiwa katika chumba maalum cha kuifadhia (cold room)  katika nyuzi joto za sentigredi 7˚C hadi 10˚C na unyevu hewa 95% na kukaa bila kuharibika kwa muda wa siku saba hadi kumi.

Vilevile unaweza kuifadhi bamia katika chumba chochote kisafi kikubwa chenye nafasi na kisicho na joto jingi chenye madirisha yanayo pitisha hewa vizuri, feni au Air conditioner kwa kupanga matenga kwa nafasi bila kuyarundika sehemu moja.

 1. Mambo Ya kuzingatia Katika Uvunaji

Bamia huweza kuharibika kwa haraka baada ya kuvunwa hivyo ni muhimu kuhakikisha haziifadhiwi kwa muda mrefu na zinafika sokoni mapema baada ya kuvunwa.

Jambo hili litawezekana kwa urahisi ikiwa mkulima wa bamia atahakikisha soko la bamia linakuwa tayari kabla ya kuanza uvunaji wa bamia.

Tuandikie Email Yako Uweze Kupata Post za Wauzaji wa Tanzania Kwa Haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo
Enable registration in settings - general