
Kutumia muda vizuri ni muhimu sana kwenye maisha Tanzania hivyo ni vyema kufahamu namna bora ya kutumia muda kwa njia yenye kuleta mafanikio.
1. Jitahidi kupanga siku yako vyema
Usikimbilie kuanza majuku yako ya siku bila kukaa chini na kutumia dakika chache za kutafakari mambo kadhaa.
Tafakari ni jambo gani muhimu zaidi ili uweze kulipa kipaumbele katika siku yako.
Jifunze kujiwekea malengo, haya yatakuwezesha kujua nini unachotakiwa kukitimiza ndani ya siku yako. Kwa njia hii utaweza kukamilisha vitu kulingana na muda uliojiwekea.
2. Jitahidi kugawanya kazi sehemu ndogo ndogo
Hili pia lipo kwenye majukumu yako ya siku; unapogawanya kazi katika vipande vidogo vidogo ni rahisi kuzitawala na kuzifanya kwa wakati.
Kumbuka pia hata kazi ngumu huwa nyepesi kama itagawanywa katika sehemu ndogo ndogo kwani utaifanya kwa urahisi ndani ya muda uliopangwa vyema.
3. Jitahidi kuweka vipaumbele vya maisha
Jifunze kupanga kazi kulingana na vipaumbele vyake, usifanye kila kitu kwa sababu ni kazi bali fanya kwa kuongozwa na vipaumbele.
Jizoeze kusema “Hapana” kwa mambo, watu au kazi zisizokuwa na umuhimu. Ukifanya hivi utatumia muda wako vyema kwenye mambo ya muhimu kwanza.
4. Jitahidi kugawa majukumu kwa watu wengine
Usifanye kila kazi kwa kuwa unaweza kuifanya. Kama una mtu au watu ambao unaweza kuwagawia majukumu fanya hivyo, kwani kwa njia hii kazi nyingi zitafanyika ndani ya muda mfupi.
Bainisha kazi zinazoweza kufanywa na wengine, andaa muongozo wa kuzifanya kisha acha watu wengine wazifanye.
5. Jitahidi upange ratiba
Watu wengi hawana ratiba rasmi ya siku, huzoea kwenda kwa mazoea tu. Jifunze kujiwekea ratiba kisha uiheshimu na kuifuata vyema.
Panga muda wa kula, kupumzika, vikao, n.k. Hili litakuwezesha kuwa na mwongozo mzuri wa namna utakavyopanga kazi zako.
Epuka kufanya mambo yasiyokuwa kwenye ratiba; ukifanya hivi utatumia muda vyema na utakuwa na maisha yenye tija zaidi.
6. Jitahidi kutenga muda wa kupumzika
Inawezekana unajitahidi kufanya kazi fulani kwa bidii ili uikamilishe kabla ya tarehe ya mwisho, lakini nini kitatokea kama utaendelea hivyo kwa muda mrefu?
Ni wazi kuwa mwili utachoka na ufanisi wako utapungua pia. Jifunze kutenga muda wa kupumzika, kwani hili litafanya mwili na akili yako kuwa katika hali bora zaidi yenye kukuwezesha kufanya kazi vyema.
7. Jitahidi kutumia muda vizuri
Ili kutumia vyema muda, unaweza kutumia kanuni ya kujiwekea ukomo wa muda unaotakiwa kutumika kwa kila kazi.
Kwa mfano unaweza kuweka kuwa kazi X inatakiwa imalizike baada ya saa 2. Ukizingatia njia hii bila kuikiuka utajikuta unatumia muda uliojiweka vyema kukamilisha kazi husika.
8. Jitahidi kupanga mapema kuhusu kesho
Kila siku fahamu kuwa kesho huandaliwa leo. Hivyo ni vyema ukaweka mikakati kadhaa ya kazi zitakazofanyika siku ya kesho.
Bainisha kitakachoanza kesho, kama kuna kazi haikukamilika leo basi panga kuikamilisha kesho kwanza.
9. Jitahidi kuondoa vinavyo ingiliana
Kuna shunguli na vitu mbalimbali vinavyoweza kuingilia utendaji wako wa kazi pamoja na matumizi yako ya muda.
Maswala kama vile mitandao ya kijamii, televisheni, miziki na filamu, mazungumzo na marafiki n.k. Ni baadhi ya mambo ambayo yasipodhibitiwa yanaweza kukupotezea muda mwingi.
Hivyo ni vyema ukajitahidi kuondoa mazingira yenye vitu tajwa hapo juu ili utumie muda wako vyema kufanya kazi zenye tija.