Jinsi Ya Kutangaza Biashara Tanzania

Jinsi ya kutangaza biashara tanzania ni swala muhimu kwa kila biashara Tanzania ila Tatizo linatokea pale ambapo biashara inashindwa kumudu gharama za matangazo, hasa matangazo ya gharama kubwa.

Naamini wewe kama mjasiriamali unafahamu kuwa kuna wakati bajeti ya biashara inakuwa imebana. Hivyo swala la kujitangaza linakuwa na changamoto.

1. Jitahidi Kutumia Tovuti

Tovuti au blog ni njia rahisi na ya gharama nafuu ya kujitangaza. Ikiwa una blog au tovuti ambayo inaidadi nzuri ya watembeleaji, unaweza kuweka tangazo la biashara yako hapo na likaonekana kwa watu wengi zaidi.

2. Jitahidi Kutumia Mitandao Ya Kijamii

Kama ilivyo wenye njia ya blog, vivyo hivyo unaweza kutumia mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Twitter na Instagram ili kujitangaza.

Kumbuka hivi leo karibu kila mtu anatumia mitandao ya kijamii. Hivyo kutangaza biashara yako kupitia kurasa au akaunti zako za mitandao hii ni rahisi na utawafikia watu wengi zaidi.

3. Jitahidi Kutengeneza Vifungashio

Siyo lazima uwe na pesa nyingi ndipo utoe zawadi au huduma ya vifungashio vyenye chapa yako. Unaweza kubuni na kuchapisha vifungashio vyenye jina na maelezo mafupi kuhusu biashara yako ili kujitangaza.

Unaweza kutoa zawadi ndogo kama vile kalamu au diary vyenye maelezo ya biashara yako.

4. Jitahidi Kutengeneza Vipeperushi

Unapopewa kadi ya kibiashara (business card) au kipeperushi lengo lake hasa ni kujitangaza. Unaweza kutengeneza kadi za kibiashara pamoja na vipeperushi vyenye maelezo mafupi kuhusu biashara yako.

Naamini njia hii ni nafuu sana kuliko kuweka tangazo kwenye televisheni wakati wa habari.

5. Jitahidi Kuwa Wakala wa Biashara Kubwa

Kuwa wakala wa biashara kubwa ni njia moja nzuri ya kujitangaza na kuongeza wateja. Mara nyingi biashara kubwa huwatangaza mawakala wao katika matangazo yao ya gharama kubwa.

Hivyo, kwa kuwa wakala wa biashara au kampuni kubwa kama vile makampuni ya simu, bima, dawa, pembejeo, au fedha; utakuwa umepata nafasi ya kutangazwa bure kabisa.

6. Jitahidi Kuhudhuria Semina na Makongamano

Njia nyingine nzuri na rahisi ya kujitangaza ni kwa kuhudhuria semina, makongamano au sehemu zenye mikusanyiko.

Uwapo katika maeneo haya, hakikisha unatafuta angalau nafasi ya kutoa salamu katika maeneo haya, ukipewa nafasi ya kuzungumza taja tu hata jina la biashara yako kwani ina maana kubwa sana.

Unaweza kuvaa pia mavazi yenye maelezo au matangazo ya biashara yako.

7. Jitahidi Kujitolea au Kutoa Misaada

Naamini mara kadhaa umewahi kuona wafanyakazi wa kampuni au biashara fulani wakitoa misaada au hata kujitolea kufanya kazi kama vile usafi wa mazingira.

Je ni nini hasa msingi wa swala hili? Kama wanauchumi wa kale walivyotangulia kusema kuwa hakuna chakula cha bure kwenye uchumi, vivyo hivyo matendo ya kujitolea au msaada yana lengo fulani.

Mara nyingi makampuni au biashara fulani zinapotoa misaada waandishi wa habari hurekodi na kutangaza habari hiyo. Hii ni njia nzuri sana ya kujitangaza.

8. Jitahidi Kuendesha Mashindano

Nani asiyependa kushinda? Naamini hata wewe unapenda kushinda zawadi fulani.

Ili ushinde unatakiwa kununua bidhaa au kusambaza habari kuhusu biashara fulani, je kwa njia hii hujaitangaza biashara hiyo? Naamini utakuwa umefanya hivyo tayari.

Unaweza kuendesha shindano dogo lenye zawadi za kawaida kama vile mikoba, vocha za simu, vinywaji, kalamu au hata bidhaa unazouza. Kwa njia hii utajitagaza kwa gharama nafuu kabisa.

9. Jitahidi Kutoa Elimu au Ushauri wa Bure

Kama kuna elimu au ushauri fulani unaoweza kuutoa ambao unaendana na biashara yako; fanya hivyo sasa.

Kwa njia hii utafahamika na kuwafikia watu wengi zaidi na hivyo kuitangaza biashara au huduma yako kwa urahisi na  kwa gharama nafuu kabisa.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo