Jinsi Ya Kupunguza Gharama Kwenye Biashara

Mbinu mojawapo ya kuongeza faida katika kampuni au biashara yako ni kwa kupunguza matumizi ya kampuni yako.

Suala la kupunguza matumizi ya pesa ni muhimu zaidi hasa pale ambapo kampuni inakuwa inakabiliwa na changamoto za kifedha.

1. Jitahidi Kupanga Upya Matumizi

Kuna matumizi mbalimbali kwenye kila kampuni lakini siyo yote ni ya muhimu. Matumizi mengine ni ya lazima lakini yamepewa kipaumbele kuliko umuhimu wake.

Kwa kupunguza matumizi ya vitu kama vile simu, umeme, maji, mafuta au hata intaneti, kutaokoa kiasi kikubwa cha pesa.

Hakikisha huduma hizi zinatumiwa vyema tena kwa matumizi ya muhimu ya kampuni na si vinginevyo.

2. Jitahidi Kupunguza Gharama za Uzalishaji

Uzalishaji wa bidhaa au utoaji wa huduma hugharimu pesa. Hata hivyo kuna mambo unayoweza kuyafanya ili kupunguza gharama za uzalishaji.

Kwa mfano kama unatumia vifungashio vya bidhaa vya bei kubwa, basi tumia vifungashio mbadala vya bei nafuu.

Inawezekana pia unatumia nishati ya umeme kufanya kila kitu, unaweza kutumia nishati mbadala kama vile umeme jua (solar) au gesi.

3. Jitahidi Kuongeza Matumizi Ya Teknolojia

Teknolojia ni muhimu sana kwa ajili ya kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni pamoja na kurahisisha utendaji kazi wa kampuni.

Ikiwa kampuni yako inatumia mawasiliano ya posta, fax, vikao vya kawaida pamoja na utunzaji wa kumbukumbu kwa njia ya karatasi, sasa ni wakati wa kuacha mifumo hiyo.

Matumizi ya barua pepe (email), mikutano kwa njia ya mtandao (online meetings), hazina pepe (cloud storages) kutapuguza gharama kubwa za uendeshaji wa kampuni.

4. Jitahidi Kuajiri Kupitia Mtandao wa intaneti

Hivi leo kampuni nyingi huajiri wafanyakazi kwenye mtandao kwa lengo kubwa la kupunguza gharama za wafanyakazi.

Unapoajiri mtu kwenye mtandao, utamlipa malipo ya kazi husika pekee, lakini unapoajiri mtu moja kwa moja ofisini kwako utamlipa gharama mbalimbali kama vile mafao, bima, gharama za uhamisho na malipo ya likizo.

5. Jitahidi Kuuza Vitu vya Zamani

Je kampuni yako ina samani, vyombo, mashine, magari, au hata vifaa vya kielektroniki kama vile kompyuta za zamani?

Badala ya kuweka vifaa hivi viharibikie ghalani (store), unaweza kuviuza kama vifaa chakavu kwa bei nafuu na ukapata pesa ambazo zingepunguza gharama za uendeshaji wa kampuni yako.

6. Jitahidi Kutafuta Watoa Huduma wa Bei Nafuu

Kuna watoa huduma tofauti na wenye gharama tofauti pia. Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni unaweza kutafuta watoa huduma kama zile za simu, mtandao au hata wale wanaokuletea bidhaa mbalimbali ambao gharama zao ni nafuu.

7. Jitahidi Kufanya Biashara Kwenye Mtandao

Biashara kwa njia ya mtandao inaweza kuzalisha faida kubwa na kupunguza kiasi kikubwa cha gharama za uendeshaji wa kampuni ikiwa itafanywa jinsi ipasavyo.

Kwa kutumia tovuti, blog au mitandao ya kijamii unaweza kujitangaza na kuwafikia wateja wengi kwa urahisi zaidi kuliko njia ya kawaida.

8. Jitahidi Kununua Vitu Kwa Jumla

Kila mfanya biashara anafahamu wazi kuwa kununua vitu kidogokidogo ni hasara zaidi kwani kodi huwa kubwa na punguzo huwa dogo.

Ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kampuni, ni muhimu kuzingatia kununua vitu kwa ujumla kuliko rejareja.

9. Jitahidi Kutumia Njia Mbadala za Matangazo

Zipo njia nyingi za kutangaza kampuni au biashara yako. Baadhi ya njia ni za gharama kubwa wakati nyingine ni rahisi na za bei nafuu.

Unaweza kutumia mitandao ya kijamii, tovuti, blog au hata vipeperushi ili kujitangaza; kwa njia hii utapunguza gharama za matangazo ya televisheni au redio.

10. Jitahidi Kulipa Madeni Kwa Wakati

Unapochelewa kulipa deni, hasa deni la taasisi za kifedha, husababisha riba kuongezeka. Jambo hili litakusababishia gharama na matumizi makubwa kwenye kampuni yako.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo