Jinsi Ya Kupata Mtaji wa Biashara Ndogo Tanzania

Jinsi ya kupata mtaji wa biashara Tanzania ni muhimu sana kwa kuwa watu wengi huanzisha biashara kwa lengo la kupata pesa ila huwa ni ngumu sana kupata mtaji.

1. Jitahidi kuweka akiba binafsi

Mara kadhaa nimekuwa nikieleza kuwa kuweka akiba kuna manufaa mengi, ikiwemo kupata uwezo wa kuwahi fursa mbalimbali na kuzifanyia kazi kwa wakati.

Hivyo basi, unaweza kutunza kiasi fulani cha pesa katika kipato chako hatakama ni kidogo, ili uweze kupata mtaji wa kuanzisha biashara au mradi wako.

2. Jitahidi kuuza mali zako

Nimewahi kukutana na watu kadhaa wakilalamika kuwa hawana mtaji, lakini ukiwachunguza sana utagundua kuwa wamezungukwa na mitaji mikubwa wasiyoitambua.

Hakuna haja yoyote ya kuwa na simu, televisheni, Kompyuta, na nguo za thamani kubwa wakati hauna mtaji wa kutekeleza mradi wako.

Unaweza kuuza vitu vyote ambavyo ukivikosa hutokufa ili uweze kupata mtaji; kumbuka uwekezaji ni muhimu kuliko maisha ya kifahari na anasa.

Ikumbukwe kuwa ukiwekeza utaweza kutengeneza pesa nyingi zaidi na kumudu kununua vitu vingine bora zaidi huko mbeleni.

3. Waombe ndugu na marafiki

Ikiwa una mahusiano mazuri na ndugu zako, wanafamilia au marafiki, kwanini unaona shida kuwaomba wakuwezeshe kupata mtaji?

Andaa wazo vizuri, tafuta watu au marafiki wakaribu watakaokuamini, waombe wakuwezeshe kupata mtaji na uwaahidi utaurejesha mapema kadri uwezavyo ili wakuamini.

Faida za mtaji au mkopo kutoka kwa marafiki na ndugu:

  • Mara nyingi hakuna riba.
  • Hakuna masharti na vigezo vigumu.
  • Upatapo shida katika biashara au mradi wako ni rahisi ndugu kukuelewa.

Kumbuka! Usicheze na mtaji wa biashara au mradi kwa kuwa umeupata kutoka kwa ndugu au marafiki; pia kumbuka kuwa mwaminifu kutimiza mapatano ili wakati mwingine usaidike.

4. Omba kuwezeshwa na taasisi

Hivi leo kuna taasisi na mashirika mbalimbali yanayotoa mitaji ya fedha na vifaa kwa wajasiriamali mbalimbali ili waweze kutekeleza mawazo yao. 

Hivi leo kuna taasisi na mashirika mbalimbali yanayotoa mitaji ya fedha na vifaa kwa wajasiriamali mbalimbali ili waweze kutekeleza mawazo yao. 

Fuatilia vyombo mbalimbali vya habari pia jiunge na vikundi vya wajasiriamali wengine ili zitokeapo fursa za mitaji uweze kuzifahamu na kuzitumia.

5. Omba mkopo kwenye taasisi za kifedha

Hivi leo ziko taasisi kedekede zinazotoa mikopo kwa ajili ya watu mbalibali; hivyo, mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha inaweza kutumiwa kama mtaji mzuri sana wa biashara. 

Hata hivyo nimekuwa nikiwashauri wajasiriamali wengi hasa wachanga kutokupendelea njia hii, ikiwa hawajaweka mikakati sahihi ya kutumia na kurejesha mkopo husika.

Hakikisha kama unataka kutumia njia hii kupata mtaji wa biashara au mradi wako, umejipanga vyema na unafahamu wazi njia na mbinu utakazozitumia kurejesha mkopo wa taasisi husika hata kama mambo yatakwenda mrama.

6. Ingia ubia na mwingine

Katika dunia yetu ya leo, wapo watu wengi wenye fedha lakini hawajapata mahali pa kuwekeza fedha zao; wengi huwa na pesa nyingi lakini hawana muda wa kuanzisha na kusimamia biashara au mradi.

Unaweza kutumia mbinu hii kupata mtaji, kwa njia ya kuingia ubia au uanahisa na mtu au watu wengine wenye mitaji wanaotafuta mahali pakuiwekeza.

Kwa mfano unaweza kumfuata mtu mwenye pesa na ukamwomba akufungulie biashara au mradi; kisha utampa asilimia fulani ya faida ya biashara au mradi huo kwa kipindi fulani hadi utakapokuwa umereejesha mtaji wake na kiasi fulani cha asante au riba.

7. Jitahidi kuchukua mali kauli

Najua umeshajiuliza ‘mali kauli’? Ndiyo, mali kauli ni njia nyingine bora kabisa unayoweza kuitumia kupata mtaji wa biashara kwa kutegemea uaminifu wako.

Zipo biashara kubwa zenye mali nyingi lakini zina mzunguko mdogo katika eneo husika; lakini inawezekana wewe unafahamu mahali ambapo mali hizo zikiuzwa zitauzika vizuri.

Unachopaswa kufanya ni kuchukua mali kwenye biashara husika na kwenda kuziuza kisha unarejesha fedha ya mauzo ya bidhaa husika na yule mwenye biashara atakupa gawio fulani kwa kazi hiyo.

Ikiwa utakuwa mwaminifu na kufanya kazi hii kwa bidii, ndani ya muda mfupi utapata mtaji wa kuanzisha biashara yako mwenyewe ambayo imetokana na kuuza mali za biashara nyingine kubwa kwa kuaminika tu (mali kauli).

8. Shindana kwenye Mashindano

Hivi leo, yanaendeshwa mashindano mbalimbali hasa yale yenye lengo la kuibua wajasiriamali wenye mawazo mazuri lakini hawana mtaji.

Kumbuka kuweka nidhamu kwenye pesa unayoipata kwenye mashindano; kwani kutokana na kupatikana kwake bila kutarajia; inaweza kutumiwa vibaya na ikapotea.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

2 Comments
  1. Nimefurahi maana nilikuwa najiuliza nitapataje mtaji wa biashara yangu ndogo ninayotaka kuanza.

Leave a reply