Jinsi Ya Kukausha na Kusindika Mihogo Tanzania

Usindikaji wa mihogo Tanzania ni muhimu sana kwasababu husaidia kupata unga ambao tunautumia kwenye matumizi ya kila siku kama chakula.

Jinsi Ya Kuandaa Mihogo

Mihogo mibichi iliyovunwa huoshwa mara mbili na oshaji wa kwanza ni ule wa kuondoa udongo wa baada ya kuvuna, na uoshaji wa pili ni baada ya kumenya mihogo kabla ya kukausha.

Baada ya kuoshwa mihogo humenywa kwa kutumia kisu kikali, na kutumbukizwa ndani ya maji safi na baada ya kumenya kiasi kinachotakiwa mihogo huoshwa na maji safi hadi kuwa meupe.

Utengenezaji wa chipsi

Mihogo iliyo safi huwekwa ndani ya mashine ya kuzungushwa kwa mikono au mashine ya kuzungushwa kwa mota ya umeme, kisha huparuliwa na kutoka vipande vidogo vidogo ambavyo huanikwa katika makaushio bora.

Mihogo Ambayo ni Michungu

Baada ya kuparuwa mihogo kuwa chipsi, huwekwa katika mifuko safi (viroba) na kuwekwa mahali penye kivuli kwa muda usiopungua saa sita ili kuacha sumu iliyoko kwenye mihogo kupotea kabla ya kukausha.

Jinsi Ya Kukausha Mihogo

Mihogo safi ambayo imeparuliwa au kukatwa vipande vidogo vidogo hukaushwa katika makaushio bora kwenye jua kali.

Makaushio bora huwa ni yale ambayo yamejengewa kichanja kilichoinuliwa mita mbili kutoka ardhini, na kutandazwa chekeche ya plastiki juu yake.

Yenye matundu madogo yasiyoweza kupitisha chembechembe za mihogo mikavu Kitambaa safi cha kaniki au mikeka safi huweza kutumika pia kama tandiko la juu ya kichanja ambapo chipsi za mihogo huweza kukaushwa kwa hali ya usafi.

Epuka kukaushia chipsi za mihogo katika majamvi mabovu juu ya ardhi kwani uchafu utakaoingia ndani ya mihogo hautakuwa rahisi kuondoa tena na husababishsa bidhaa ya unga kutokuwa na ubora.

Ukaushaji Duni wa Mihogo

Uharibifu au upotevu unaosababishwa na ukaushaji duni [wa kienyeji]unatokana na muhogo kubadilika rangi na na kupata ukungu.

Njia Bora za Kukausha Mihogo

Mihogo iliyoparuliwa (chipsi) hukaushwa na baadaye kusindikwa ilikupata unga.

Vifaa na Malighafi za Kusindika Mihogo

 • Mihogo safi
 • Kisu kikali kisichoshika kutu.
 • Mashine ya kuparua (grater)
 • Kaushio bora
 • Kitambaa cheusi kikubwa cha kutosha na kilicho safi au majamvi safi
 • Vifungashio.

Jinsi Ya Kutengeneza Makopa Ya Mihogo

 • Menya mihogo safi kuondoa maganda.
 • Parua kwa kutumia mashine kupata chipsi.
 • Anika kwenye kichanja au kaushio bora lilotandikwa kitambaa cheusi kilicho safi au jamvi safi ili kuzuia uchafu kuingia ndani ya chipsi.
 • Sambaza na geuzageuza vipande hivyo ili kuharakisha ukaukaji.
 • Muda wa kukausha hutegemea hali ya jua na ukubwa wa vipande. Vipande vidogo hukauka upesi na huwa bora kwa mlaji. Vipande vikubwa huchelewakukauka na hupoteza ubora
 • Fungasha vipande vilivyokaushwa kwenye magunia safi, kisha hifadhi kwenye maghala bora.

Jinsi Ya Kuhifadhi Mihogo

Njia pekee ya kuhifadhi mihogo kwa muda mrefu ni kwa kuhifadhi mihogo iliyokaushwa. Muhogo uliokaushwa huweza kuhifadhiwa kwa muda wa miezi 6 hadi 12 bila kuharibika.

Makopa yanashambuliwa na dumuzi zaidi kuliko chipsi, hivyo inashauriwa kuhifadhi mihogo iliyoparuliwa na kukaushwa (chipsi) ambayo inakuwa katika hali ya unga unga na kufanya mashambulizi ya dumuzi yapungue kabisa.

Chipsi za mihogo zinaweza kuhifadhiwa katika magunia safi ya juti na kupangwa ndani ya ghala juu ya chaga.

Pia chipsi zinaweza kuhifadhiwa katika hali ya kichele ndani ya sailo au kihenge bora. Mihogo haihifadhiwi kwa kutumia madawa ya viwandani.

Hifadhi kwa hali ya ukavu, usafi na kagua ghala mara kwa mara kuona kama kuna mashambulizi ya panya na chukua tahadhari kuepuka upotevu wa chakula hicho.

Hifadhi kwa muda ulioshauriwa ili kudumisha ubora wa bidhaa.

Vifaa Vya Kusindika Muhogo Uliokaushwa

 • Mashine ya kusaga
 • Mifuko ya kufungasha
 • Mashine ya kufungia mifuko
 • Chekeche

Jinsi Ya Kusindika Muhogo Uliokaushwa

 • Saga muhogo uliokaushwa kwenye mashine ili kupata unga.
 • Chekecha kwa kutumia chekeche laini. Ukubwa wa matundu ya chekechekeche hutegemea kiwango cha ubora wa unga kinachotakiwa na soko.
 • Weka unga kwenye mifuko kutegemea matakwa ya soko (kilo 1,2,5,10, au 50)
 • Funga vyema kwenye mifuko ya kufungashia ili hewa isiingie
 • Hifadhi kwenye chaga au fremu zilizowekwa mahali pakavu na pasipokuwa na mwanga mkali.

Matumizi Ya Unga wa Muhogo

Unga wa mhogo hutumika kupika ugali, uji na katika kutengeneza maandazi, tambi, keki, biskuti, kababu, donati, mkate, chapati na chapati maji.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply