Jinsi Ya Kufanikiwa Kujifunza Kingereza Tanzania

Kujifunza kingereza kunaweza kuwa ni kugumu lakini inawezekana na Kusoma Kiingereza inawezekana lakini kuna mambo kadhaa unatakiwa kuyafahamu na kuyafanya kwa uhakika.

1. Jitahidi Kupenda Kingereza

Ili uweze kufanya au kujifunza kitu chochote ni lazima kwanza ukipende. Ikiwa unataka kufahamu Kiingereza kwa muda mfupi ni lazima ukipende kwani ndipo utaweza kujifunza kila mara bila kuchoka wala kukata tamaa.

Jikumbushe manufaa utakayoyapata baada ya kufahamu Kiingereza vizuri.

2. Jitahidi Kujifunza Kingereza Kila Siku

Huwezi kufahamu Kiingereza kama hutojifunza kila siku. Hakikisha unaongeza misamiati, unajifunza matamshi pamoja na kanuni mbalimbali za lugha.

Mambo ya kukumbuka hapa:

  • Nunua kamusi ya Kiswahili na Kiingereza.
  • Soma vitabu na machapisho mbalimbali yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza.
  • Tumia tovuti za kujifunza lugha kama vile Duolingo, Babbel, BBC Learning English n.k. kujifunza Kiingereza.
  • Kama inawezekana, tafuta mwalimu au chuo cha kujifunza Kiingereza.

3. Jitahidi Kuzungumza Kiingereza

Huwezi kumudu kuzungumza Kiingereza kama hutozungumza. Jitahidi katika kutumia Kiingereza katika mazungumzo yako hata kama utakosea.

Jifunze maneno uliyoyazoea kuyatumia mara kwa mara na uyafahamu kwa Kiingereza ili uyatumie katika mazungumzo.

Jambo la kuzingatia ni kuangalia tu mtu unaye ongea naye; ikiwa mtu hajui Kiingereza basi usitumie Kiingereza kwani anaweza kuona unamdharau.

Hata kama huna mtu wa kuzungumza nae, unaweza kuzungumza mwenyewe tu kwa sauti ndogo bila shida; kwani ni mambo mangapi unayokuwa unanayawaza na kuyajadili akilini mwako peke yako? Anza kuzungumza sasa.

4. Jitahidi Kujifunza Kuandika Kingereza

Kuandika kwa Kiingereza kutakusaidia sana kuboresha uwezo wako wa Kiingereza cha kuandika. Ikiwa unaandika ujumbe, machapisho (posts) kwenye mitandao ya kijamii, kadi, au hata shajara (diary); basi tumia lugha ya Kiingereza.

5. Jitahidi Kuacha Kuogopa Kukosea

Ni rahisi mtu kushindwa kujifunza Kiingereza kwa kigezo tu cha kuogopa kufanya makosa. Makosa ni hatua muhimu katika kujifunza kitu chochote.

Unapofanya makosa na kuyabaini, ni wazi kuwa mbeleni hutoyarudia tena. Hivyo, tumia Kiingereza katika kila eneo bila kuogopa kufanya makosa.

6. Jitahidi Kutazama Vipindi vya English

Najua wengi ni wafuasi wa miziki na filamu; miziki na filamu za Kiingereza zinaweza kukusaidia kwa kiasi kikubwa kujifunza lugha.

Usipende kutazama filamu zilizotafsiriwa; jitahidi kujifunza maana za maneno unayosikia kwenye filamu na miziki kwa kutumia kamusi niliyoitaja kwenye hoja namba moja.

Jitahidi pia kutazama vipindi au hotuba mbalimbali zilizoandaliwa kwa lugha ya Kiingereza kupitia televisheni au mtandao wa YouTube.

Jifunze jinsi watu wanavyotamka maneno pamoja na kuchunguza maana zake.

7. Jitahidi Kuwaza Kwa Kingereza

Kuwaza kwa Kiingereza? Ndiyo, kuwaza kwa Kiingereza kutaongeza uwezo wako wa lugha kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano badala ya kuwaza “Nitakwenda mjini kesho…” unaweza kuwaza “I will go to town tomorrow…”.

Kufanya hivi kutakujengea uwezo wa kutumia na kufahamu Kiingereza zaidi.

8. Jitahidi Kuelewa na Usikariri Kanuni

Kila lugha ina kanuni zake. Usipoteze nguvu kubwa kukariri kanuni, bali elewa matumizi ya kanuni zinazotawala mpangilio wa maneno na matumizi yake.

Kwa mfano sentensi nyingi za Kiingereza huwa na (Mtenda-Tendo-Mtendwa au Kitendwa) yaani (Subject-Verb-Object)

Mf. Mary killed the dog.

John is cooking the food.

Kufahamu kanuni kama hii na nyinginezo, kutakuwezesha kuelewa kwanini mtenda huanza kisha kufuatiwa na tendo pamoja na mtendwa au kitendwa katika sentensi za Kiingereza.

9. Jitahidi Kutafuta Rafiki

Ikiwa kuna mtu ambaye mnaweza kujifunza kwa pamoja, basi mshirikishe ili mjifunze kwa pamoja. Au ikiwa kuna mtu anamudu vyema Kiingereza, unaweza kumwomba akusaidie katika mchakato wako wa kujifunza.

Kwa kufanya hivi utaweza kuuliza maswali au hata kuzungumza moja kwa moja na mshirika wako. Kama wewe ni mtumiaji mzuri wa mtandao, unaweza kupata mshirika kwenye mtandao pia.

10. Jitahidi Kuwa na Subira na Usikate Tamaa

Ni wazi kuwa zipo chngamoto katika kujifunza lugha mpya hasa Kiingereza. Lakini ni muhimu ukafahamu kuwa ni swala la muda, uvumilivu, mazoezi na nia tu ndivyo vitakavyokuwezesha kufahamu Kiingereza vyema.

Hakuna kitu kizuri kinachotokea kwa usiku mmoja, fanya bididi usikatishwe tamaa na changamoto; nawe kwa hakika utafikia lengo.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply