
Watu wengi hawafahamu umuhimu wa kupumzika, ndiyo maana hawatengi muda wa kutosha wa kupumzika.
Ni ukweli usiopingika kuwa kupumzika kuna manufaa makubwa sana kwenye miili na utendaji wetu wa kazi kila siku.
1. Kupumizika Huongeza Uwezo wa Kumbukumbu
Ubongo wa mwanadamu unahitaji kupumzika ili uweze kujijenga na kufanya kazi vyema. Ikiwa mtu hatapata muda wa kutosha wa kupumzika, uwezo wake wa kutunza kumbukumbu utapungua.
Pia utafiti uliofanyika umebaini kuwa kutokupumzika huongeza kiasi fulani cha protini kwenye ubongo ambacho huchangia katika kutokea kwa maradhi ya Alzheimer (Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu).
2. Kupumizika Huondoa Hatari Ya Kupata Kiharusi
Kiharusi ni ugonjwa unaosababishwa na kupasuka kwa mishipa midogo ya damu kwenye ubongo; hili husababisha damu kuvuja ndani ya ubongo.
Utafiti uliofanyika umebaini kuwa uchovu hasa ule unaoambatana na msongo wa mawazo, unaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo na kisha kusababisha ugonjwa wa kiharusi.
3. Kupumizika Hulinda Afya Ya Moyo
Kupumzika kuna manufaa makubwa kwenye afya ya moyo wako. Ni wazi kuwa kasi ya usukumaji wa damu wakati wa kufanya shughuli mbalimbali ni tofauti na wakati unapokuwa umepumzika.
Hivyo basi, unapopata muda wa kupumzika unaupa moyo wako nafasi ya kupunguziwa mzigo wa kusukuma damu kwa kasi, ambao umeubeba wakati ulipokuwa unafanya shughuli mbalimbali.
4. Kupumizika Hutoa Muda wa Mwili Kujijenga
Miili yetu inahitaji kujijenga kila mara hasa baada ya shughuli nyingi. Kwa njia ya kupumzika utaweza kuupa mwili wako nafasi nzuri ya kujijenga na kurejeshha tena nguvu iliyotumika wakati wa shughuli mbalimbali.
5. Kupumizika Huongeza Hamasa Ya Utendaji
Nani anapenda kufanya kazi akiwa amechoka? Naamini hakuna. Kupata muda wa kutosha wa kupumzika kutakuwezesha kujisikia vizuri na kuwa tayari kutekeleza majukumu yaliyoko mbele yako.
Ikiwa basi unataka kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, ni muhimu kuhakikisha unapata muda wa kutosha wa kupumzika.
6. Kupumizika Huimarisha Misuli
Tunapopumzika misuli yetu inajijenga na kurudisha ute wake uliopotea wakati wa shughuli mbalimbali. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kila baada ya kazi tunapata muda wa kutosha wa kupumzika ili tuboreshe afya za miili yetu.
7. Kupumizika Huimarisha Kinga Mwili
Kinga mwili ni muhimu sana kwani hutuwezesha kukabiliana na magonjwa. Kwa njia ya kupata muda wa kutosha wa kupumzika tunatoa nafasi kwa mfumo mzima wa kinga mwili kujijenga na kujiimarisha.
8. Kupumizika Huondoa Msongo wa Mawazo
Chanzo kimojawapo cha msongo wa mawazo ni uchovu, na chanzo kimojawapo cha maradhi mbalimbali ni msongo wa mawazo.
Hivyo ni muhimu kuhakikisha tunapumzika ili akili na fikra zetu zijisafi na kutuepusha na tatizo la msongo wa mawazo.
9. Kupumizika Hutuwezesha Kula Vizuri
Ni ukweli usiopingika kuwa tukiwa tumechoka hatuwezi kula vizuri. Hivyo kupata muda mzuri na wakutosha wa kupumzika kutakuwezesha kula chakula vyema.
10. Kupumizika Huepusha Ajali za Barabarani
Je ulishasikia ajali zilizosababishwa na madereva wanaosinzia? Uchoovu na kukosa muda wa kupumzika (hasa kulala) humfanya mtu akose utulivu na uwezo wa kumudu chombo anachoedesha.
Hivyo ni muhimu kwa madereva na watu wote wanaotumia vyombo vya usafiri kuhakikisha wanapata muda mzuri na wakutosha wa kupumzika.