Faida za Kukosea Kwenye Maisha

Faida za kukosea kwenye maisha ni muhimu kuzifahamu na unaweza kujifunza kutokana na makosa mbalimbali unayoyafanya kila mara maishani mwako.

1. Makosa Hutuonyesha Mambo Tusiyoyafahamu

Ni wazi kuwa makosa mengine hutokea kwa kufanya vitu au maamuzi tusiyoyafahamu vyema. Kwa njia ya makosa hayo tutaweza kufahamu vitu hivyo.

2. Makosa Hutufundisha Maana Ya Mafanikio

Pasipo shaka, mafanikio siyo mteremko au ukamilifu. Mafanikio ni kujifunza kutokana na makosa na kuepuka kuyarudia tena mbeleni.

Kupitia makosa tunaweza kujifunza tufanye nini ili tufanikiwe katika lile tunalolifanya.

3. Makosa Hutufundisha Kuomba Msaada

Tunapofanya makosa, mara nyingi tunatambua kuwa tunahitaji watu wakutusaidia kuyarekebisha au kutupa ushauri. Kabla ya kufanya kosa ambalo limekuletea matatizo, unaweza kufikiri unajitosheleza au hauhitaji msaada wowote.

4. Makosa Hutuwezesha Kufahamu Mambo Ya Msingi

Inawezekana kosa limetokea kutokana na kufanya au kuzingatia jambo ambalo siyo la msingi. Hivyo kwa njia ya kosa hilo utaweza kubaini mambo ya msingi na yasiyo ya msingi.

5. Makosa Hutufundisha Umuhimu wa Wengine

Inawezekana umekosea kwa sababu umepuuza nafasi ya watu wengine katika maamuzi au kile unachokifanya. Kwa sababu hii basi utakuwa umefahamu umuhimu wa wengine.

6. Makosa Hutuonesha Kinachofaa na Kisichofaa

Unapotumia kitu au njia fulani na ikakusababishia kukosea, ni wazi kuwa utakuwa umebaini kuwa kitu au njia hiyo haifai.

7. Makosa Hutufundisha Thamani Ya Msamaha

Ikiwa umemkosea mtu ambaye ni wa thamani kwako, ni wazi kuwa utahitaji kumwomba msamaha ili kuendeleza uhusiano wako na yeye.

Hivyo kwa njia ya makosa tunatambua umuhimu wa msamaha.

8. Hutufundisha kufanya uchaguzi sahihi

Mara nyingi tunakosea kutokana na kufanya uchaguzi mbaya. Hivyo kosa litakufundisha kuwa uchaguzi uliofanya siyo sahaihi.

9. Makosa Hutufundisha Kufanya Majaribio

Unapofanya kosa na kupata matokeo fulani ni sawa na mtu anayefanya majaribio. Hivyo utafahamu matokeo ya kile ulichokifanya kama ni mazuri au mabaya.

10. Makosa Hutuwezesha Kufanya Chaguzi Nyingine

Inawezekana kuna uchaguzi fulani uliupuuzia au hukufahamu umuhimu na ubora wake. Baada ya kukosea katika uchaguazi ulio uchagua utabaini kuwa uchaguzi ulioupuuzia una nafasi kubwa.

11. Makosa Hutuonyesha Madhaifu Ya Mfumo

Kosa hutuwezesha kubaini ni wapi kuna udhaifu katika maisha yetu au jambo tunalolifanya. Kwanjia hii tutaweza kurekebisha udhaifu huu ili tuwe na tija zaidi.

12. Makosa Hutukumbusha Kuwa Tunafanana na Wengine

Mara nyingi tunapofanikiwa tunajisahau kuwa tuko sawa na wengine. Lakini tunapokosea tunafahamu kuwa tunapaswa kuthamini wengine kwani nasi tuna madhaifu kama wao.

13. Makosa Hutufundisha Kuwa na Unyenyekevu

Mtu anapokosea mara nyingi huwa mpole na mnyenyekevu; hii ni kutokana na kutambua udhaifu au mapungufu aliyoyafanya. Hivyo makosa ni njia bora kabisa inayoweza kutufundisha na kutufanya kuwa wanyenyekevu.

14. Makosa Hutufundisha Muda Sahihi wa Kufanya Mambo

Makosa mengine hutokea kwa sababu maamuzi au jambo limefanywa nje ya wakati. Kwa kupitia kosa, tunaweza kujifunza ni wakati gani stahiki tunapaswa kufanya jambo au maamuzi fulani.

15. Makosa Hutuonyesha Matatizo Kwenye Mahusiano

Matatizo kwenye mahusiano hubainika hasa pale mtu mmoja anapomkosea mwingine.

Kila upande utajitahidi kutaja na kuonyesha matatizo yaliyopo kwenye mahusiano husika ili kuficha kosa; hivyo kwa njia hii makosa yatawezesha kubaini matatizo yaliyoko kwenye mahusiano.

16. Makosa Hutufundisha Ubunifu

Makosa hutufanya tuwe wabunifu zaidi ili tuweze kuyakabili wakati mwingine.

17. Makosa Huwa ni Kitahadharishi

Kutokea kwa kosa fulani leo, kunaweza kuwa kunakutahadharisha dhidi ya hatari au kosa lingine kubwa la mbeleni.

18. Makosa Hutukumbusha Juu Ya Ubinadamu

Binadamu ni kiumbe dhaifu kinachokosea. Kwa njia ya makosa tunakumbushwa kuwa sisi ni binadamu, tena tuna udhaifu na hatujakamilika.

19. Makosa Hutufundisha Kuwa Mafanikio Siyo Kila Kitu

Ikiwa unafanikiwa kila mara, ni rahisi kujiaminisha kuwa mafanikio ndiyo kila kitu kwenye maisha. Lakini utakapofanya makosa na kushindwa utabaini kuwa bado maisha yanendelea kama kawaida.

20. Makosa Hutufundisha Kutumia Muda Vyema

Kuna makosa yanayotokana na matumizi mabaya ya muda. Hivyo kuyafanya au kuyafahamu, kutakufundisha umuhimu wa matumizi mazuri ya muda.

21. Makosa Hutufundisha Kuwa na Subira

Unapokosea, itakubidi upate muda wa kufanya tena au kutatua kosa ulilolifanya kabla ya kupata kile ulicholenga.

Hivyo kwa njia hii tunaweza kujifunza kuwa na subira na uvumilivu.

22. Makosa Hutufundisha Kutokukata Tamaa

Huwezi kujifunza kutokukata tamaa kama haupiti kwenye changamoto; na mara nyingi ikiwa changamoto hizo zinatokana na makosa uliyoyafanya.

23. Makosa Hutufunza Kutumia Pesa Vyema

Mara nyingi tunakosea kutokana na kushindwa kutumia pesa vyema. Tunapokuwa kwenye matatizo kutokana na makosa ya matumizi mabaya ya pesa tutajifunza kuwa wakati mwingine inatupasa kutumia pesa vyema.

24. Makosa Hutufundisha Kutazama Malengo

Kuna umuhimu mkubwa sana wa kujiwekea malengo vyema maishani. Lakini tunapokwama, moja kwa moja tunajifunza jinsi ya kuyabadili au kuyaboresha vyema wakati mwingine.

25. Makosa Yanatuonesha Marafiki Sahihi

Ikiwa utafanya kosa kutokana na aina ya marafiki ulio nao, ni wazi kuwa kosa hilo litakufundisha umuhimu wakutazama aina za watu au marafiki unaoshirikiana nao.

Marafiki bora watakutia moyo na kukuhamasisha kuendelea mbele ili kutimiza malengo yako na siyo kukuzamisha.

Tuandikie Email Yako Uweze Kupata Post za Wauzaji wa Tanzania Kwa Haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply

Wauzaji
Logo