Changamoto za Mwanzoni Kwenye Biashara

Ukianza biashara yoyote Tanzania changamoto za mwanzoni Kwenye Biashara ni nyingi sana na ni muhimu kufahamu changamoto za biashara ndogo ndogo.

1. Mwanzoni Kwenye Biashara Utahisi Maumivu

Kila mtu aliyefanikiwa amepitia kwenye safari yenye maumivu na ikumbukwe kuwa kupita njia yenye changamoto ndiko hutuelekeza kwenye mafanikio.

Jifunze kutumia changamoto na maumivu kuwa kama hamasa ya kufanya juhudi zaidi kufikia mafanikio. Hakuna haja ya kulalamika na kukata tamaa bali anzia ulipo kwenda mbele ili kukamilisha malengo yako.

2. Mwanzoni Kwenye Biashara Utatamani Kukata Tamaa

Wengi waanzapo safari ya mafanikio huanza kwa kasi kubwa kwani wao hufikiri tu juu ya mafanikio. Lakini katika ukweli halisi ni kuwa, mwanzoni kuna changamoto lukuki ambazo usipotazama malengo yako ni rahisi kukata tamaa.

Kipindi hiki kimekuwa kigumu sana kwa watu wengi kwani hawaoni ile nuru ya awali tena bali wanaona changamoto kila kukikucha. Kumbuka wahenga walisema “mwanzo ni mgumu”; jitahidi usirudi nyuma nawe utaona matokeo yake.

Mambo ya kufanya kama unataka kukata tamaa:

  • Uliza waliokutangulia walifanyaje kutatua hizo changamoto unazoziona.
  • Soma vitabu na makala mbalimbali za kukuhamasisha.
  • Jikumbushe juu ya malengo yako na matokeo utakayoyapata utakapokuwa umevuka kwenye hizo changamoto.

3. Mwanzoni Kwenye Biashara Utapoteza Mahusiano na Watu

Katika safari ya kuelekea kufanikiwa mambo mengi hutokea, kama vile kupoteza fedha, vitu, na watu.

Kumbuka kuwa siyo watu wote watakaoweza kwenda pamoja na wewe katika safari hii, kwani kuna wengine hawana hamasa uliyo nayo, hawapendi ufanikiwe, wana mambo au shughuli zao.

Hivyo usishangae hata watu wa karibu uliokuwa unawategemea wakakuacha bila msaada wowote au wakabadilika sana.

Jipe moyo, fanya bidii tambua mnufaika wa kwanza wa mafanikio yako ni wewe wala sio wao.

4. Mwanzoni Kwenye Biashara Utakatishwa Tamaa

Katika njia ya mafanikio kuna watu wachache sana wenye mawazo chanya na wanaopenda mafanikio yako. Hivyo basi, utakutana na watu wengi sana watakao kukatisha tamaa na kukutisha ili urudi nyuma.

Utawasikia wakisema hili hautafanikiwa, hili halikufai, fulani alifanya akashindwa au halinipi faida. Jambo la kufanya hapa ni kulinda fikra na nafsi yako visipokee mawazo na misimamo ya hawa watu kwani kwa kufanya hivi utaweza kutazama tu lengo lako na kufanya bidii kulifikia.

5. Mwanzoni Kwenye Biashara Utachukiwa Bila Sababu

Kwa hakika binadamu hapendi mafanikio ya mwingine, moyo wake hujaa chuki, maumivu na husuda pale mwingine anapofanikiwa.

Wapo watu wanaotamani ubaki kama ulivyo na usiweze kufanya kitu cha kuwazidi wao au walichoshindwa kukifanya.

Nimeshuhudia marafiki zangu kadhaa wakipunguza uhusiano na mimi pale waliponiona nimepata mafanikio kadhaa hasa kuwazidi wao.

Hivyo basi, badala ya kupambana na wenye wivu na chuki pambana na malengo yako, kisha mafanikio yako yatawapa somo.

6. Mwanzoni Kwenye Biashara Utajilaumu Mwenyewe

Kujilaumu hakuepukiki katika safari ya mafanikio hasa pale unapokuwa umepata tatizo au hasara kwa uamuzi ulioufanya hapo awali.

Kwa hakika, huwezi kubadili uamuzi au tendo lililopita badili uelekeo wa maisha yako ya baadaye kuanzia ulipo.

Usijilaumu tena kwani utauwa ile hamasa yako ya ndani na hutoweza kufikia mafanikio yako.

Subscription Form

Tuandikie email yako uweze kupata post za mtandao wa wauzaji kwa haraka.

Tuandikie Mawazo Yako

Leave a reply